HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 27, 2023

SMZ yazidi kuimarisha huduma za Afya vijijini

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  inaendelea kuimarisha huduma za Afya mijini na vijijini  ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025 na azma ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 yenye lengo la kuwapatia huduma bora  za kijamii wananchi wake bila ya ubaguzi wa aina yoyote ikiwemo huduma ya Afya.

Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla ameyasema hayo wakati akifungua Kituo cha Afya cha Uzi na Ng'ambwa ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za kutimia miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

 

Amesema kuwa ili nchi iwe na uchumi Imara na maendeleo endelevu ni lazima wananchi wake wawe na Afya bora itakayowapa nguvu za kufanya shuhuli zao ambazo zinawapatia kipato pamoja na kukuza uchumi wa nchi.

 

Mhe.Hemed  amesema kituo cha  afya cha Uzi na Ng'ambwa kilichojengwa na fedha za Mradi Tasaf  kwa kushirikiana na Serikeli ya Mpinduzi ya Zanzibar kimekamilika kwa kiwango kilicho bora na asilimia ndogo iliyobakia Serikali itatoa fedha kwa ajili ya umaliziaji ili wananchi wapatiwe huduma bora na kwa wakati stahiki.

 

Makamu wa pili wa Rais amemuagiza Waziri wa Afya kuhakikisha madaktari watakaotoa huduma katika kituo cha Afya Uzi na Ng’ambwa  lazima waishi maeneo ya karibu na kituo hicho ili kuweza kuwahudumia  wagonjwa kwa masaa  ishirini na nne (24).

 

Aidha ameitaka Wizara ya Afya  kuandaa utaratibu wa kutafuta Vijana wenye Taaluma ya Afya wa maeneo ya Uzi na Ng’ambwa  ama kuwasaidia kuwasomesha  kada mbali mbali za Afya ili kuwaandaa kufanya kazi katika kituo hicho mara baada ya kumaliza masomo yao jambo ambalo litaondoa usumbufu na uhaba wa madaktari katika vituo vya afya.

 

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka wananchi wa Uzi na Ng’ambwa  kutoa ushirikiano kwa serikali pamoja na madaktari wanaotoa huduma katika kituo hicho na vituo vyengine ili kuweza kutoa huduma zilizobora na kufikia malengo ya serikali ya kuwapatia huduma bora wananchi wake bila ya kujali tofauti za aina yoyote.

                                     

Nae Waziri wa Afya Mhe Nassor Ahmed Mazurui amesema Jengo limekamilika na limekidhi viwango vyote vya kuitwa kituo cha Afya  ambacho kitatoa huduma za matibabu ya aina mbali mbali zikiwemo  za mama na mtoto.

 

Amesema Wizara itahakikisha inalitunza jengo hilo ili liweze kutoa huduma zilizo bora pamoja na kufikia azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kutoa huduma bora kwa wananchi wote bila ya kujali itikadi zao sambamba na kuwajengea nyumba za makaazi  Madaktari watakaofanya kazi katika kituo hicho ili kuwarahisishia ufanyaji wa kazi zao.

 

Akitoa taarifa za kitaalamu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili, Sera, Uratib na Baraza la Wawakilishi Dkt. Islam Seif Salum amesema Ujenzi wa Kituo cha  Afya cha Uzi na Ng'ambwa kimejengwa na Mradi Tasaf kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar na Wananchi wa Uzi na Ng’ambwa ambacho kimegarimu zaidi ya Milioni mia tatu na sitini (360) hadi kukamilika ambacho kitatoa huduma za Afya kwa wananchi wa Uzi na Ng'ambwa.

 

Amesema kuwa kituo hicho kitotoa huduma  mbali mbali za matibabu ikiwemo ya Uzazi, matibabu ya meno, mama na mtoto na huduma za maabara ambazo zitatolewa kwa masaa 24 kwa wananchi wote.

 

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohamed Mahmoud amesema wananchi wa Uzi na Ng'ambwa wanaishukuru Serikali ya Awamu ya Nane (8) inayoongozwa na Rais wa Dkt Hussein Mwinyi  kwa kuwajengea kituo cha Afya ambacho kitawaondolea usumbufu wa kufuata huduma za Afya masafa ya mbali.

 

Amesema kuwa dhamira ya Dkt Mwinyi ni kukuza Uchumi kwa kujenga Misingi  Imara ya Kiuchumi ambayo itaendelea kuifungua Zanzibar kiuchumi hivyo ni lazima kuhakikisha anawawekea mazingira maziri wananchi wake ikiwemo upatikanaji wa huduma za afya kwa wakati na kwananchi wote bila ya kujali itikadi za aina yoyote.

 

No comments:

Post a Comment

Pages