Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk. Delila Kimambo (kushoto), akitoa maelezo kwa wafanyakazi wa Idara ya Wateja Wadogo na Biashara wa benki ya NMB walipofika kutoa mchango wao wa Sh. 11.5 za kusaidia gharama za matibabu ya Watoto wenye uhitaji wanaotibiwa katika taasisi hiyo. (Na Mpiga Picha Wetu).Kaimu Mkuu wa Idara ya Wateja Binafsi wa Benki ya NMB, Ally Ngingite (kulia), akikabidhi sehemu ya msaada wa vifaa tiba kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe, Dk. Yona Kabata (kushoto) vilivyotokana na michango ya wafanyakazi wa Idara ya Wateja Wadogo na Biashara ya benki hiyo. Wa pili kushoto ni Muuguzi wa hospitali hiyo, Flora Mchaina, Meneja Mikopo ya Nyumba Benki ya NMB, Miranda Lutege (wa pili kulia) na Meneja Mahusiano Mwandamizi NMB, Pendo Massawe (katikati). (Na Mpiga Picha Wetu).
NA MWANDISHI WETU
WAFANYAKAZI wa Idara ya Wateja Wadogo na Biashara ya Benki ya NMB, wameikabidhi Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ya Dar es Salaam, kiasi cha Sh. Mil. 11.5 kusaidia kulipia gharama za matibabu ya watoto wenye uhitaji wanaotibiwa hapo, huku wakitoa vifaa tiba vyenye thamani ya Sh. Mil. 1.7 kwa Wodi ya Watoto ya Hospital ya Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani.
Kwa nyakati tofauti Jumanne ya Desemba 19, Kaimu Mkuu wa Idara ya Wateja Binafsi wa NMB, Bw. Ally Ngingite, alikabidhi kwa niaba ya wafanyakazi hao, hundi ya mfano ya kiasi hicho kwa Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi JKCI, Dk. Robert Aloyce na vifaa tiba hivyo kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe, Dk. Yonna John Kabata.
Akizungumza wakati wa hafla ya jijini Dar es Salaam, Ngingite, alibainisha kuwa kiasi walichotoa kimetokana na michango ya wafanyakazi wa Idara hiyo na nyongeza kutoka benki yake, lengo likiwa ni kugusa maisha ya wenye uhitaji katika jamii, ambapo hufanya hivyo kila mwisho mwaka kupitia idara mbalimbali na Ofisi za Matawi yao kote nchini.
"Kwa niaba ya wafanyakazi wenzetu, tuko hapa kutoa kiasi cha shilingi 11,570,000 kilichotokana na michango ya mishahara yetu na nyongeza kutoka taasisi yetu, lengo likiwa ni kugusa maisha ya watoto wenye uhitaji wanaotibiwa hapa. Tunajua matatizo ni mengi na wenye uhitaji ni wengi, lakini tukaona tuje hapa kusaidia wachache kati yao.
"Tumaamimi kwa kiasi hiki tunachokabidhi, tutakuwa tumeyagusa na kuokoa maisha ya watoto walio katika 'stage' mbalimbali za matibabu hapa JKCI, ili waweze kufanyiwa upasuaji na baada ya hapo tunawaombea uponaji wa haraka kuwawezesha kuendelea na maisha yao ya kawaida.
"Hii yote ni kusapoti uwekezaji mkubwa ulilofanywa na Serikali katika Sekta ya Afya, tumepita idara mbalimbali kujionea hilo na sisi kama wadau tukajiona tunao wajibu na uwezo wa kuunga mkono hilo.
"Tumekuwa tukifanya hivi kila mwisho wa mwaka kwa wafanyakazi wa benki yetu kupitia Idara na Ofisi za Matawi kote nchini kujichanga mishahara yao na kuangalia maeneo ya kusaidia iwe kwa mayatima ama wagonjwa kama hivi," alibainisha Bw. Ngingite.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa taasisi hiyo, Dk. Delila Kimambo, aliishukuru NMB kwa msaada waliotoa kwa watoto hao wanaotibiwa na taasisi yake na kwamba, kiasi hicho kinaenda kugusa pakubwa mioyo na maisha ya wanufaika miongoni mwa watoto wanaotibiwa hapo.
"Mlichofanya hapa ni jambo kubwa, mmewapa watoto hawa na wazazi ama walezi wao, mwisho mzuri wa mwaka, tayari kwa kuingia mwaka mpya na matumaini mapya.
"Kwa niaba ya watoto hawa, sisi JKCI tunawashukuru wafanyakazi wote na NMB kwa ujumla kwa kuisapoti Serikali ambayo imefanya uwekezaji mkubwa sana hapa unaopaswa kuungwa mkono na wadau wa afya kama hivi mlivyofanya nyie" alisema Dk. Delila.
Kwa niaba ya watoto wengine, Pili Khalfan wa Maneromango mkoani Pwani, ambaye ni mama mzazi wa mmoja wa watoto walionufaika, alisema msaada huo umekuja kwa wakati, kwani alielemewa na gharama za matibabu kiasi cha kukata tamaa, hasa baada ya kutengwa na ndugu pamoja na kukimbiwa na baba wa mtoto wake.
"Naishukuru sana NMB kwa kunipa aina hii ya msaada, ambao sikuutarajia na sitousahau maishani mwangu. Nimeteseka sana, sikuwa na msaada wowote, hata ndugu walinitenga, huku baba wa mtoto wangu naye akinikimbia.
"Nimekuwa napata wakati mgumu, kulala kwangu shida, kula yangu na mtoto ni shida. Aliwahi kutokea mfadhili wa kusaidia matibabu ya mtoto, lakini bima aliyokatiwa tukaambiwa ni ndogo, hivyo haitoshi kugharamia upasuaji wa moyo.
"Leo NMB inaenda kunifuta machozi mimi na mwanangu kusaidia gharama za matibabu yake. Naitakia mafanikio yaliyotukuka benki hii, ili iweze kuendelea kusaidia wenye uhitaji wengi zaidi," alisema Pili wakati akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wazazi na walezi wenzake.
Kutoka Kisarawe, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya hiyo, Dk. Yonna John Kabata, hakusita kuipongeza NMB kwa msaada wa vifaa tiba, ambavyo sio tu vitawasaidia watoto hospitalini hapo, bali pia utawapa wepesi katika kuhudumia makundi ya watoto wanaotakiwa kufanyiwa oparesheni (surgery cases) na wale wanaohitaji matibabu ya kawaida (treatment cases).
"Kwa niaba ya uongozi wa Hospitali na wagonjwa wote, nitumie nafasi hii kuwashukuru sana NMB kwa msaada huu wa vifaa tiba, ambavyo mnaweza kuona ni mdogo, ila niwahakikishie ni mkubwa na huenda ingetuchukua muda mrefu kuvipata.
"Hapa zipo baadhi ya huduma za bure kwa watoto, lakini wahitaji ni wengi, hivyo huongeza changamoto ya kuishiwa vifaa na mwingine kuvikosa. Hii isiwe mara ya mwisho, mtukimbilie kila mtapokuwa na fungu la kusaidia, itaokoa maisha ya wagonjwa wetu," alisema Dk. Kabata, mbele ya Muuguzi Mfawidhi, Sista Barikian Ngona na Muuguzi wa Wodi ya Watoto, Flora Mchaina.
Mwisho
No comments:
Post a Comment