Muonekano wa Daraja la Mazinyungu katika barabara ya Rudewa-Kilosa lenye urefu wa KM 22.5 linalojengwa Wilayani Kilosa,Mkoani Morogoro.
Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Morogoro Mhandisi Lazeck Kyamba na Mshauri Mwelekezi Mhandisi Protus Mwasyoke alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Rudewa Kilosa yenye urefu wa KM 22.5 Mkoani Morogoro.
Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amemtaka mkandarasi Reynolds Construction Company (RCC), anayejenga barabara ya Kidatu- Ifakara km 66.9 na daraja la Ruaha lenye urefu wa mita 133 kuhakikisha ujenzi wa barabara na daraja hilo unakamilika ifikapo Machi mwaka huu.
Kukamilika kwa daraja hilo linalounganisha wilaya za Kilosa na Kilombero mkoani Morogoro kutafungua uchumi wa wakazi wa mikoa ya Morogoro, Njombe, Iringa na Ruvuma kwa kuwa inapita kwenye eneo lenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na biashara.
“Kwa kuwa katika ujenzi huu hakuna changamoto ya fedha hivyo katika miezi miwili ijayo hakikisheni kazi hii inakamilika na wananchi wananufaika na uwekezaji huu mkubwa uliofanywa na Serikali”, amesema Eng. Kasekenya.
Amezungumzia umuhimu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kushirikiana na mkandarasi kuhakikisha alama muhimu za usalama barabarani zinawekwa mapema iwezekanavyo ili kuepusha ajali kwa watumiaji wa barabara hiyo na kuhakikisha magari yatakayotumia barabara hiyo hayazidishi uzito.
Kwa upande wake meneja wa TANROADS mkoa wa morogoro Lazeck Kyamba amemhakikishia Naibu Waziri Kasekenya kuwa watamsimamia mkandarasi huyo ili kazi zifanywe usiku na mchana na hivyo kukamilika katika muda mfupi ujao.
Nae mkuu wa wilaya ya Kilombero Dastan Kyobya amesema kukamilika kwa daraja la ruaha na barabara hiyo kutaleta fursa nyingi za kiuchumi kwa wakazi wa wilaya hiyo na kuipongeza TANROADS kwa usimamizi mzuri na shirikishi kwa wananchi.
Katika hatua nyingine naibu waziri kasekenya amekagua barabara ya mikumi-kilosa hadi dumila ambayo ujenzi wake unaendelea kwa awamu na kumtaka mkandarasi Umoja JV anaejenga sehemu ya Rudewa-Kilosa km 22.5 kukamilisha madaraja matatu ya Mazinyungu, Kobe na Wailonga yaliopo mjini Kilosa ili kukamilisha mradi huo na kuwawezesha wananchi kunufaika na mradi huo.
Naibu Waziri Kasekenya yuko mkoani Morogoro kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja na kusisitiza umuhimu wa watumiaji wa barabara kuzingatia sheria ili kuilinda miundombinu hiyo ili idumu kwa muda mrefu.
No comments:
Post a Comment