NA VICTOR MASANGU, KIBAHA
Baraza
la madiwani katika Halmashauri ya mji Kibaha limeiomba serikali
kuwaundia mamlaka yao ya maji safi ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa
kuwahudumia wananchi kwa urahisi zaidi na kuondokana na changamoto
zinazowakabili.
Hayo
yamebainishwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji Kibaha Mhe Mussa
Ndomba kwa niaba ya madiwani wenzake wakati wa kikao cha baraza la
madiwani kipindi cha robo ya pili.
Mhe.Ndomba
alisema kwamba kwa sasa katika baadhi ya maeneo kumekuwa na changamoto
ya upatikanaji wa maji safi na salama hali ambayo inawapa wakati mgumu
wananchi kupata huduma hiyo.
Alifafanua
kwamba katika halmashauri ya mji kibaha kuna Hospitali ya Lulanzi
ambayo ni ya Wilaya lakini nayo inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa
maji hususa kwa wakinamama wanaojifungua kupata shida sana.
"Kutokana
na hali hii ya changamoto ya maji tunaiomba serikali kutusaidia katika
halmashauri ya Kibaha tuwe na mamlaka yetu ya maji ambayo itakuwa ni
msaada mkubwa kwa wananchi wetu ukizingatia maji yote yanatokea kwetu
Kibaha,"alifafanua Ndomba.
Aidha
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa endapo Kibaha ikiba ikiwa na mamlaka
yake itaweza kusaidia kuwapunguzia wananchi adha ambayo yamekuwa
wakiipata.
Pia alisema
kwamba kwa sasa halmashauri ya mji Kibaha imetenga kiasi cha shilingi
milioni 60 kwa ajili ya kuhakikisha inaboresha miundombinu ya maji ili
iweze kufika katika Hospitali ya Lulanzi ili wagonjwa waondokane na
kuangaika katika suala la maji.
Kadhalika
Mwenyekiti huyo aliziomba taasisi wezeshi zote kuwa na ushirikiano wa
pamoja katika masuala ya kutekeleza miradi mbali mbali ya kimaendeleo
ili kuepusha usumbufu unaokuwa ukijitokeza katika utekelezaji wa miradi.
Mwenyekiti
huyo alimpongeza kwa dhati Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kuamua kulifuta shirika la Elimu kibaha na kumuomba awapatie
ardhi kutoka eneo hilo kwa ajili ya kulipanga na matumizi mengine ya
kimaendeleo.
"Kiukweli
Rais wetu amesikia kilio chetu cha siku nyingi kwa kuamua kulifuta
shirika la elimu Kibaha na sisi siku nyingi kama madiwani tulikuwa
tunaomba kupatiwa eneo kwa lengo la shughuli mbali mbali lakini
hatukuweza kulipata,"alibaisha Ndomba.
Katika
hatua nyingine Ndomba aliwataka watumishi na watendaji kuhakikisha
wanatimiza wajibu wao kwa kusimamia kumaliza migogoro ya ardhi.
"Kero
nyingi zinazokuja ni kuhusiana na migogoro ya ardhi ya wakati mwingine
unakuta mkurugenzi anashughulikia migogoro hiyo ya ardhi ya asilimia 90
kitu ambacho kilitakiwa kimalizike katika ngazi za chini sio hadi ifike
kwa mkuu wa Wilaya au mkuu wa Mkoa,"alisema Ndomba.
Nao
baadhi ya madiwani aliohudhuria katika kikao hicho walisema katika
maeneo yao kumekuwa na uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara hasa
katika kipindi cha mvua hivyo mamlaka husika zinapaswa kufanya
matengenezo.
Aidha
waliongeza kuwa suala la changamoto ya maji bado ni tatizo katika maeneo
yao hivyo kuanzishwa kwa mamlaka yao kutaweza kuwa ni mkombozi mkubwa
kwa wananchi.
Kikao cha
baraza la madiwani katika halmashauri ya mji Kibaha kimekutana katika
robo ya pili kwa ajili ya kujadili mipango mbali mbali ya kimaendeleo
katika sekta tofauti,changamoto zilizopo pamoja na kuweka mikakati ya
kuzitafutia ufumbuzi kupitia serikali pamoja na taasisi wezeshi.





No comments:
Post a Comment