HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 27, 2024

CHUO KIKUU MZUMBE CHAPONGEZWA KUWEZESHA WAJASIRIAMALI KUPATA MIKOPO KWA URAHISI

Kamishna wa Idara ya Maendeleo Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha Dkt. Charles Mwamwaja amewapongeza chuo kikuu Mzumbe kwa kubuni njia mbadala ya kupata mikopo kwa wajasiriamali wadogo kupitia mfumo wa mikopo kutoka kwa watu wengi kwa njia ya mtandao.


Kamishna Mwamwaja ameyasema hayo leo tarehe 25 Januari 2024, jijini Arusha katika kongamano la kimataifa la wajasiriamali wanaonufaika na mikopo kutoka kwa watu wengi inayosimamiwa na Chuo Kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na Shirika la kuhudumia Viwanda vidogo(SIDO) kwa udhamini wa Shirika la kimataifa la Maendeleo la Denmark (Danida Fellowship Center) ambapo jumla ya wajasiriamali mia moja wameweza kupata mikopo iliyowanufaisha kuanzisha na kuendeleza biashara katika mikoa ya Arusha, Tanga, Dar es Salaam, Morogoro na Mbeya.


Amesema serikali inaamini nafasi ya kijana katika kuwaendeleza na kutengeneza mazingira wezeshi ili kujikwamua kiuchumi na kutengeneza ajira kupitia biashara wanazoanzisha hivyo fursa ya mikopo isiyohitaji dhamana isiyohamishika ni muhimu kwa chachu ya maendeleo kwa Taifa.


Amewataka wataalamu wa Biashara na mikopo jumuishi kutoa matokeo ya tafiti wanazozifanya badala ya kuzifungia makabatini ili zijulikane kwa watu wengi na kufanya biashara kuwa pana zaidi kwa chachu na maenedeleo ya taifa kwa ujumla.


“Mikopo hii isiyokuwa na dhamana na riba nafuu haina kikwazo kwa mkopaji na ni njia bora zaidi ya kuongeza kipato kwa watu wengi hususan vijana kwani kwa utafiti uliofanywa unaonesha wamiliki wa nyumba hawazidi asilimia kumi hivyo kusaidia kuondoa vikwazo kwa waajasiriamali wadogo” alisisitiza Dkt. Mwamwaja.


Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi huo, Mhadhiri Mwandamizi kutoka Skuli ya Biashara Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Nsubili Isaga amesema matokeo ya utafiti wa mradi huo  yamekuja na njia mbadala ambayo mjasiriamali anakopa kwa njia rahisi na ya kwanza nchini Tanzania kwa kupata mtaji kwa njia ya mtandao.


“Ni kama kuchangishana kwenye harusi au misiba, hii ni njia nyingine ambayo wakopeshaji wako wengi huko duniani ambao wanavutiwa na wazo lako na kukuchangia” alisema Dkt Isaga.


Amesema matokeo ya utafiti huo umeshirikisha SIDO ambao ndio wenye dhamana ya kutoa mikopo kwa wajasiriamali na kwamba kupitia SIDO walipatikana wafanyabiashara ambapo walipewa mikopo na mafunzo kutoka katika mikoa ya Dar es salaam, Tanga, Mbeya, Morogoro na Mwanza.


Aidha, Dkt. Isaga ametoa wito kwa vijana kujiunga na Shirika la viwanda vidogo SIDO ambao wanadhamana ya kulea wajasiriamali sambamba na kuwahimiza wale wanaopata mikopo kurejesha kwa wakati ili wengine waweze kunufaika.


Awali akifungua kongamano hilo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Profesa William Mwegoha amesema utafiti huo umeweza kuangalia maeneo mbalimbali kwa vijana kupata mitaji ya kuendeleza biashara zao kwani hupitia mradi huu, chuo kinakuwa sehemu ya jitihada za serikali za kutafuta mitaji kwa ajili ya kuwainua wajasiriamali nchini.


Profesa Mwegoha ameshukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt.  Samia Suhulu Hassan inayohimiza umuhimu wa vijana katika mendeleo ya kiuchumi, ikilenga kuwawezesha kujiajiri kupitia sekta ya maendeleo ya fedha.


“Serikali inajitahidi kutoa mazingira mazuri kwa vijana kupitia mitaji ya kuanzisha au kuendeleza biashara na inaongeza fursa za ajira kwa vijana kupitia michango ya mtandaoni hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi katika sekta mbalimbali. Alisisitiza Prof. Mwegoha


Tunaamini kuwa mradi huu ni wa mafanikio kutokana na ushirikiano wa wizara ya fedha na Chuo kikuu Mzumbe kwa kuwa unaongeza uendelevu wa upatikanaji wa fedha za kuanzishia au kukuza biashara za vijana wajasiriamali kupitia wanataaluma wa Chuo Kikuu Mzumbe ambao tayari wameshanolewa katika uandishi wa miradi ya tafiti.

No comments:

Post a Comment

Pages