HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 01, 2024

INDIA-TANZANIA FRIENDSHIP RUN YAFANA DAR ES SALAAM

*Dk. Ndumbaro asema 2024 itakuwa 'Bab kubwa' kupigwa Hifadhi ya Kitulo Njombe



NA TULLO CHAMBO-RT

MBIO maalum za kwanza za kujenga urafiki kati ya nchi za India na Tanzania 'India-Tanzania Friendship Run, zimemalizika kwa mafanikio makubwa kwenye viwanja vya Green, Dar es Salaam, Desemba 31, 2023 huku ikibainishwa kuwa zitakuwa endelevu.

 

Mbio hizo zilipambwa na Nyota nguli wa India, Milind Soman, zilianza Desemba 30 kwa mbio za Km 5 na 10 Desemba 30 na kuendelea zile za masafa marefu 'Ultra Marathon' Km 130 kutoka Dar hadi Mji wa Kihistoria wa Bagamoyo mkoani Pwani na kurejea Dar, ambako washiriki wakiwa na Milind walirejea viwanja vya Green Desemba 31 na kupokelewa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Damas Daniel Ndumbaro na Balozi wa India Tanzania, Binaya Pradhan.


Katika Ultra Marathon ambako 'Super Star' huyo wa kimataifa kutoka India mwenye miaka 58 mbali na kushiriki yeye, mkewe na mama yake mzazi, alisindikizwa na wakali wa mbio za masafa kutoka klabu mbalimbali kama Goba Road Runners, Wasafi FM Jogging na nyinginezo.


Akizungumza wakati wa kufunga mbio hizo, Dk. Ndumbaro, alisema kufanyika tukio hilo ni sehemu ya utekelezaji wa mikataba iliyofikiwa kutokana na ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan nchini India Oktoba, 2023.


Dk. Ndumbaro, alibainisha kuwa, Rais Samia akiwa India, Serikali za pande zote mbili ziliingia mikataba miwili, moja katika sekta ya Utamaduni kwa miaka mitano na mwingine katika michezo ambao ni wa muda mrefu. Waziri Dk. Ndumbaro, alibainisha kuwa wizara imeanza kutekeleza kwa vitendo ambapo ni kuanza kwa tukio hilo.


Mbali na Super Star Milind katika maisha yake kufanya vema katika radha hususan kwenye marathon, pia ana rekodi katika uogeleàji, uigizaji filamu na mwanamitindo, ambako katika ziara yake hiyo nchini alifanya warsha na sekta hizo ikiwemo ile ya uigizaji Tanzania 'Bongo Movie' na India 'Bollywood'.


Dk. Ndumbaro mbali na kupongeza kamati zote za maandalizi, alisema 2024 tukio hilo litakuwa kubwa zaidi, ambako litafanyika wiki ya kwanza ya Julai katika hifadhi ya Taifa ya Kitulo na kulitaka Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), kuliweka katika kalenda yake ya matukio.


Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa RT, William Kallaghe, mbali na kushukuru serikali za India, Tanzania na wadhamini mbalimbali waliofanikisha tukio hilo, alisema limeleta hamasa na mafanikio makubwa katika mchezo wa riadha, mojawapo kwa upande wa Ultra Marathon ambao bado hamasa yake haijawa kubwa hapa nchini.


Moja ya mafanikio, ni pamoja na ushirikiano wa kiufundi ambako Super Star huyo kutoka India, Milind, ameahidi kumleta mtaalamu wa Ultra Marathon kubadilishana mawazo na kutoka elimu kwa wataalamu wa Tanzania.


Katika kuhitimisha tukio hilo, ilitolewa hundi ya Sh. Milioni 5, ambapo Kallaghe, alibainisha itakwenda kwa kuanzia kwa baadhi ya nguli wa zamani walioliletea Taifa sifà katika mchezo wa riadha,wanaofanya vizuri hivi sasa hususan waliofanikiwa kufuzu kuiwakilisha Tanzania katika michezo ya Olimpiki Paris 2024 na vijana wanaofanya vema hivi sasa.

No comments:

Post a Comment

Pages