Na Mwandishi Wetu
Waziri
wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye
(Mb) amesema wizara imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha
inawekeza na kukuza matumizi ya TEHAMA nchini.
Ameyasema hayo,
leo Januari 26, 2024 wakati akishuhudia utiaji saini wa hati ya
makubaliano ya ushirikiano kati ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na
Teknolojia ya Habari na Benki ya NMB uliofanyika katika Hoteli ya Serena
jijini Dar es Salaam.
"Hafla hii ya utiaji saini wa hati ya
ushirikiano kati ya wizara na NMB inaweka historia na kuthibitisha kuwa,
TEHAMA na mabadiliko ya kidigitali nchini ni masuala mtambuka
yanayogusa Sekta ya Umma, Sekta Binafsi na wananchi kwa ujumla, amesema
Mhe. Nape.
Mhe. Waziri Nape ameeleza kuwa utekelezaji wa
ushirikiano huu unalenga Serikali na Sekta Binafsi inakuwa na mifumo
bora na rafiki ya utoaji wa huduma kwa wananchi inayotumia teknolojia za
kisasa, mazingira wezeshi ya kutumia TEHAMA nchini na kuhakikisha
tunakuza vipaji vya vijana kwenye masuala ya TEHAMA.
Kwa upande
mwingine ushirikiano huu unalenga kuongeza idadi ya vituo vya ubunifu
katika maeneo mbalimbali ya nchini na eneo la ujumuishi wa kifedha wa
kidigitali kwa kuongeza wigo wa utumiaji wa fedha kwa njia ya
kidigitali.
Akitoa salamu za Benki ya NMB Afisa Mtendaji Mkuu wa
Benki hiyo Bi. Ruth Zaipuna amesema kuwa kwa muda mrefu Benki ya NMB
imekuwa mshirika mkubwa wa Serikali katika kuchagiza Sera ya Uchumi wa
Kidigitali, pamoja na kuunda na kuboresha mifumo mbalimbali ya TEHAMA.
Amesema
kuwa Benki ya NMB imewekeza na kuwa Benki yenye Kituo cha Kutunza
Taarifa (Data Center) ya kisasa, mifumo imara na ya kisasa ya TEHAMA,
Teknolojia za kisasa za kulinda usalama wa mifumo na taarifa za Benki na
za wateja wake na mifumo ya kisasa ya kusaidia ubunifu.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bwana
Mohammed Khamis Abdullah amesema wizara imeshirikiana na NMB katika
masuala mbalimbali ikiwemo uandaaji wa Mkakati wa miaka 10 wa uchumi wa
kidigitali, uandaaji wa Sera Mpya ya TEHAMA ya 2024 na ujenzi wa mfumo
wa kuwatambua wateja (eKYC - electronic Know Your Customer).
"Tumeanza
maandalizi ya kutayarisha Sheria ya TEHAMA nchini baada ya kukamilika
kwa Sera ya TEHAMA 2024 ambayo ipo kwenye hatua za mwisho za
uidhinishwaji",alisema Katibu Mkuu huyo.
Hafla ya utiaji saini wa
hati ya makubaliano ya ushirikiano kati ya Wizara ya Habari,
Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Benki ya NMB imewakutanisha
maafisa waandamizi wa wizara na wataalam wa TEHAMA waliiongozwa na Bw.
Mohamed Mashaka ambaye ni Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Mifumo na Huduma
za TEHAMA na kwa NMB waliongozwa na Bw. Kwame Makundi, Afisa Mkuu wa
Teknolojia na Mabadiliko ya Kidigitali wa Benki ya NMB.
No comments:
Post a Comment