Na Mwandishi Wetu
BAADA ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Zambia kesho timu ya Taifa, Taifa Stars itashuka dimbani kumenyana na DR Congo katika mchezo wa mwisho wa Kundi F kwenye fainali za mataifa ya Afrika AFCON 2023.
Sare hiyo dhidi ya Zambia licha ya kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Morocco imeipa ‘Stars’ pointi ya kwanza ambayo imeifanya kuwa na nafasi ya kufuzu hatua ya 16 bora kulingana na msimamo wa kundi F ulivyo.
Ingawa Taifa Stars inashika mkia katika kundi hilo na pointi yake moja, inaweza kufuzu hatua ya 16 bora ikiwa itaibuka na ushindi katika mechi ya mwisho dhidi ya DR Congo na Zambia ikashindwa kupata ushindi dhidi ya Morocco.
Lakini hata Zambia ikishinda, Taifa Stars inaweza kufuzu ikiwa itaifunga DR Congo kupitia nafasi nne zinazotolewa kwa timu zilizoshika nafasi ya tatu zikiwa na matokeo bora kwenye makundi.
Katika mechi ya leo, Taifa Stars ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Saimon Msuva katika dakika ya 12 kabla ya patson Daka kuisawazishia Zambia katika dakika ya 88.
Kwa sasa Morocco inaongoza kundi F ikiwa na pointi nne, ikifuatiwa na DR Congo na Zambia ambazo kila moja ina pointi mbili na Taifa Stars iko mkiani ikiwa na pointi moja.
No comments:
Post a Comment