HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 19, 2024

Elimu ya Fedha kuingizwa Mitaala ya Elimu ya Juu kuwajengea vijana nidhamu

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga amesema Serikali itahakikisha elimu ya fedha inaingizwa kwenye mfumo rasmi wa elimu na kuanza kufundishwa nchini.


Amebainisha hayo jijini Dar es Salaam wakati akifungua warsha ya siku tatu kuhusu uingizaji wa elimu ya fedha katika mitaala ya elimu ya juu iliyowakutanisha viongozi mbalimbali na taasisi za elimu ya juu nchini ambapo jambo hilo litatekelezwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Elimu, Seyansi na Teknolojia na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Amebainisha kuwa elimu hiyo itatolewa katika vyuo vikuu lengo likiwa ni kuwawezesha vijana kuwa na uwezo wa kuwa na nidhamu ya kusimamia fedha, kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria  kujenga uelewa  wa masuala ya fedha  kwa jamii.

“Wizara tutahakikisha elimu ya fedha inafundishwa katika mfumo wa elimu nchini hivyo twende kwa haraka kuhakikisha vijana ambao ni sehemu ya jamii nchini wanakuwa na uelewa wa masuala ya fedha hivyo natarajia wakuu wa vyuo mtabeba uelewa   huo muhimu kwa vyuo vyetu nchini,” amesema Kipanga.

Naibu Waziri Kipanga amebainisha kuwa, BoT, itaendelea kusimama na vyuo na  taasisi za elimu na Wizara ya Elimu katika kuhakikisha dhana ya elimu hiyo inakuwa endelevu na inafundishwa katika ngazi za jamii hata  kwa wale walio nje ya mfumo rasmi wa elimu nchini.

Ametumia fursa hiyo kuviagiza Vyuo Vikuu  nchini kushirikiana na BoT kufanya tathmini ya utekelezaji  wa mpango huo ili kuboresha mbinu na nyenzo za kufikisha ujumbe  huo kwa jamii.

Hivyo amesema baada ya tathmini hiyo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ipatiwe taarifa ili isaidie katika kufanya maamuzi kwani Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kujenga uelewa wa masuala ya fedha kwa jamii.
Kwa upande wake, Naibu Gavana wa BoT, Sauda Msemo amesema  elimu ya fedha inakuwa ni sehemu ya masomo, kwmaba somo hilo liingizwe kwenye mfumo ya elimu msingi hadi vyuo vikuu.

Kwamba Aprili mwaka jana,  BoT iliwashirikisha wakuu wa taasisi za Elimu ya Juu nchini, kwa  uwakilishi wa wakuu wa  vyuo vikuu pamoja na TCU na NACTIVET kwa lengo la  kukubaliana juu ya azma ya kufundisha somo la elimu ya fedha  ngazi ya elimu ya juu nchini.

“Hadi hivi sasa taasisi tatu za elimu ya juu zimechukua hatua za kuingiza somo la elimu ya fedha katika mitaala yao, hivyo warsha hii ni kuchochea uwepo wa elimu  ya fedha kwa vyuo vingi nchini  kuendana na mabadiliko ya mageuzi ya kiuchumi nchini,”amesema Msemo.

Msemo ameeleza kwamba, takwimu ya Sensa ya Watu na  Makazi ya Mwaka 2022 inaonesha takribani watu asilimia 34.5 ni vijana  walio na umri kati ya miaka 15-35 hivyo ili kuleta tija na ufanisi katika masuala ya uchumi,  ujuzi na uzoefu wa masuala ya fedha ni moja ya sifa muhimu kufikia azma hiyo.

Amesema elimu hiyo ya fedha kwa Watanzania itachochea maendeleo kwa  kuongeza utumiaji rasmi wa huduma za fedha  na  kuwawezesha watu wengi kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi ya kifedha na kuendesha shughuli zao kwa ufanisi na kukuza uchumi kwa ujumla.

Sauda amesema elimu kwa vijana wa vyuo vikuu itawasaidia kuweka akiba, kupanga bajeti na kufanya uamuzi wa masuala ya fedha kwa kuzingatia viashiria hatarishi na kuelewa taasisi mbalimbali zinazotoa huduma za fedha ili kufanya maamuzi sahihi ya fedha ili waitawale.

"Tunatarajia kujenga ‘displine’ ya fedha kupitia elimu ya fedha kwani watakuwa na uwezo wa kutawala fedha sio  fedha kuwatawala vijana hao,” ameongeza Msemo.

Kadhalika amesema  BoT kwa kushirikiana na wadau wengine  wa Baraza la Huduma Jumuishi  za Fedha, imetoa muongozo  na mtaala wa elimu ya fedha  kwa wakufunzi  ambao utatumika na taasisi za elimu ya juu kwa kuwafundisha watoa huduma  za elimu ya fedha kuwafikia wananchi wote walio nje  mfumo wa elimu.

“Tayari tumeingia makubaliano na baadhi  ya taasisi zaa elimu katika mtaala  huo wa kufunzi wa fedha na tulioingia nao makubaliano ni Chuo Kikuu cha Iringa, Zanzibar, Chuo Kikuu cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania ,” ameseama.

Kwa upande wake, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine Morogoro (SUA), Felix Adam amesema warsha hiyo ni muhimu kwake kwa sababu hayo maeneo yanayojadiliwa yatawasaidia kuwapa elimu ya fedha wahitimu wao.

No comments:

Post a Comment

Pages