HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 26, 2024

MICHUANO YA MEI MOSI YAFIKIA HATUA YA NUSU FAINALI

Na Eleuteri Mangi, Arusha

 

MICHUANO ya Michezo ya Mei Mosi 2024 imefikia hatua ya nusu fainali katika michezo ya mpira wa miguu na netiboli ambapo kwa mwaka huu taasisi 54 zinashiriki mashindano hayo.

 

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo ya Mei Mosi Taifa Bi. Roselyne Massam wakati akiongea na waandishi wa Habari kuhusu michuano hiyo inayoendelea jijini Arusha ikiwa ni shamrashara za kuelekea maadhimisho ya sikukuu  ya Wafanyakazi Duniani

 

 “Tunategemea kilele cha michezo hii kufanyika Aprili 29, 2024 ambapo tutapata washindi wetu watakaopewa zawadi na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi)" amesema Bi Massam.

 

Kwa upande wa mpira wa miguu, timu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeichapa Wizara ya Maliasili na Utalii magoli 2-0, huku timu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wamewafunga Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa magoli 4 -1, nayo Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wamewaliza timu ya Wizara ya Maji kw bao 1 – 0 na timu ya  Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi imesonga mbele kwa kuwashinda Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa penalti 4–2. Timu hizo zilitoka suluhu katika dakika za kawaida.

 

Katika mchezo wa netiboli, timu ya Ofisi ya Rais Ikulu wameifunga  Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa jumla ya magoli 64 – 20, nayo Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi imewashinda TAMISEMI kwa magoli 46–22; huku  Wizara ya Ulizi na Jeshi la Kujenga Taifa wameichezesha kwata Wizara ya Uchukuzi kwa kuwafunga  magoli 63–18 na Wizara ya Afya wameifunga timu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa magoli 76 – 21.

 

Katika kuimarisha undugu na ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao ya kila sekta binafsi, Bi Massam amewahimiza waajiri kuwaruhusu watumishi wao kufanya mazoezi wakati wote wanapokuwa kwenye vituo vyao vya kazi hatua itakayowafanya kuleta ushindani wakati wa mashindano ya Mei Mosi na mashindano ya mashirikisho ya SHIMIWI, BAMATA, SHIMISEMITA na SHIMMUTA.sz

No comments:

Post a Comment

Pages