HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 26, 2024

WATUMISHI WA UMMA WAASWA KUWEKEZA KABLA YA KUSTAAFU



Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Omolo, akizungumza wakati akifunga mkutano wa 37 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Natu El Maamry Mwamba, uliofanyika katika ukumbi wa Kilimanjaro, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini Dar Es Salaam.

Baadhi ya Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha kutoka mikoa mbalimbali wakifuatilia hoja zilizokuwa zikijadiliwa katika mkutano wa 37 wa Baraza la Wafanyakazi mwaka 2023/2024, uliofanyika katika ukumbi wa Kilimanjaro, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar Es Salaam. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Dar es Salaam)

 

Na Asia Singano   -  WF, Dar es Salaam

 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bi. Jenifa Omolo amewataka watumishi wa Umma kutimiza majukumu yao kwa wakati na weledi na kuwekeza kwa ajili ya Maisha ya uzeeni ili kuepuka usumbufu katika kipindi cha kustaafu.

Bi. Omolo ametoa wito huo wakati wa mkutano wa 37 wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Fedha mwaka 2023/2024, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, katika ukumbi wa Kilimanjaro, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar Es Salaam.

‘’Ni vyema ukamaliza majukumu yako kwa wakati husika ili angalau miezi miwili kabla ya kustaafu kila kitu chako kiwe sawa siyo mpaka siku chache kuelekea kustaafu bado una majukumu mengi hujayakamilisha”, alisema Bi. Omolo.

Alisisitiza kuwa ni vyema watumishi wakawekeza wakati wakiwa kazini ili kuhakikisha kuwa wanakuwa na uwezo wa kuendesha maisha na kukidhi mahitaji yao muhimu baada ya kustaafu.

‘’Mada ya uwekezaji ni muhimu sana kama ilivyowasilishwa wafikishieni watumishi wote umuhimu wa kuwekeza, tunaweza kuwekeza UTT AMIS, NIC na Benki lengo ni kuhakikisha kuwa tunavyofanya kazi tuwe na namna ya kuwekeza kwa ajili ya familia zetu na kujiandaa kustaafu’’, alisisitiza Bi. Omolo

Aliongeza kuwa Uongozi wa Wizara hiyo utahakikisha kuwa unatatua changamoto mbalimbali zinazoweza kukwamisha utendaji wa watumishi na kuhakikisha wanapata stahiki.

Aidha Bi Omolo amewataka watumishi hao kushiriki kikamilifu katika kutekeleza bajeti iliyopitishwa kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali za kuleta maendeleo ya nchi.

Mkutano wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara ya fedha hufanyika kila mwaka ambapo hutoa fursa kwa watumishi kujadili  na kuwasilisha changamoto mbali mbali katika maeneo ya kazi ili ziweze kutatuliwa.

No comments:

Post a Comment

Pages