HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 26, 2024

SIMBA QUEENS SIO SHIDA ZAO


NA JOHN MARWA


Wakati kikosi cha Wanaume cha Simba SC kikipitia nyakati ngumu katika mashindano mbalimbali msimu huu. Dada zao wa Simba Queens hizo sio shida zao kwani wameendeleza ubabe wa Ligi Kuu ya wanawake (WPL) mbele ya Yanga Princess kwa kuifunga mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi hapo jana.


Mabao ya Simba Queens yaliwekwa kimiani na Asha Mnunka katika dakika ya 49 na 90 kumfanya afikishe mabao 15 kwenye ligi nyuma ya kinara Stumai Abdallah mwenye mabao 17, huku bao la tatu likifungwa na Jentrix Shikangwa katika dakika ya 66 na kumfanya afikishe mabao matano. Bao la kufutia machozi la Yanga limefungwa na Mmarekani Kaeda Wilson.


Simba imeifunga Yanga mara mbili kwenye ligi msimu huu ikiipiga kwa idadi ya mabao hayo hayo ambayo straika wake Mnunka aliwafunga mabao mawili-mawili katika kila mechi na hivyo kuiwezesha Queens kuifunga Princess jumla ya mabao 6-2.


Wakati Simba Queens wakifanya hivyo, Kaka zao wao wameteseka kwa kukubali kipigo cha jumla ya mabao 7-2 katika michezo miwili msimu huu dhidi ya watani zao Yanga SC. Ni kama watani wamebadilishana kiitikio msimu huu japo wimbo mtunzi ni yule yule.


Timu hizo mbili kwenye dakika 15 za mwanzo kipindi cha kwanza na pili zilionyesha ushindani wa aina yake na kila timu ilifika langoni kwa mwenzie lakini Simba ilikuwa bora zaidi katika dakika 15 za pili na dakika 15 za mwisho katika kila kipindi.


Matokeo hayo yanaifanya Simba iendelee kukaa kileleni na pointi 34 huku Yanga ikiendelea kukaa nafasi ya tatu na pointi 21.

No comments:

Post a Comment

Pages