HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 21, 2024

INEC YAWATAKA WATENDAJI WA UBORESHAJI KUTUNZA VIFAA

 Na Mwandishi wetu, Kigoma


Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetaka watendaji wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura Mkoani Kigoma kuhakikisha wanatunza vifaa vya uandikishaji ili vikaweze kutumika maeneo mengine nchini.

 

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegeke wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa Waratibu wa Uandikishaji wa mkoa, Maafisa Waandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na Maafisa TEHAMA wa halmashauri yaliyoanza leo tarehe 20 hadi 21 Juni,2024 Mkoani Kigoma.

“Kwa kusisitiza, ni muhimu kutekeleza majukumu yenu kwa umakini katika kila eneo ikiwemo utunzaji wa vifaa vya uandikishaji hasa ikizingatiwa kuwa, vifaa hivi vimenunuliwa kwa gharama kubwa sana na vinatarajiwa kutumika katika maeneo mengine ya uandikishaji nchini,” alisema Jaji Mwambegele.

Amesema kutokuwa makini katika utunzaji wa vifaa hivi kutapelekea athari kubwa katika ukamilishaji wa zoezi hili muhimu na amewataka kuzingatia maelekezo yote yatakayotolewa na Tume ili muweze kuyafanyia kazi wakati zoezi litakapokuwa limeanza.

Aidha, Jaji Mwambegele amesema matokeo bora ya zoezi hili yanategemea uwepo wa ushirikiano mkubwa kati ya watendaji wote wa uboreshaji, serikali, vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi.

“Ninawasihi muwe na ushirikiano mzuri na wa karibu na Tume wakati wote mtakapokuwa mnatekeleza majukumu yenu na ikiwa mnahitaji ufafanuzi au maelekezo yeyote, msisite kuwasiliana na Tume,” alimema Jaji Mwambegele.

Mapema kabla ya kuanza mafunzo hayo, washiriki walikua kiapo cha kujitoa uanachama na kile cha kutunza siri mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Rose Kangwa.

Mafunzo hayo yanahusisha namna ya ujazaji wa fomu pamoja na kutumia mfumo wa kuandikisha wapiga kura (Voters Registration System - VRS) ili waweze kupata uelewa wa pamoja utakaowapa fursa ya kutumia kwa ufasaha mfumo huo pamoja na vifaa vingine vya kuandikisha wapiga kura.

“Mafunzo haya, yanawajengea umahiri wa kuwafundisha Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Kata kisha nao watatoa mafunzo hayo kwa Waendeshaji wa Vifaa vya Bayometriki na Waandishi Wasaidizi ambao ndio watahusika na uandikishaji wa wapiga kura vituoni,” alisema Jaji Mwambegele.

Aidha, Maafisa TEHAMA watapatiwa mafunzo maalum ya jinsi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiufundi (Troubleshooting) endapo zitajitokeza wakati wa zoezi la uandikishaji wa wapiga kura vituoni.

Katika hatua nyingine, Jaji Mwambegele amewaambia watendaji hao kuwa  wakati wa uboreshaji wa Daftari mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura jambo ambalo litasaidia kuleta uwazi katika zoezi zima lakini pia mawakala hao watasaidia kutambua waombaji wa eneo husika hivyo kupunguza kutokea kwa vurugu zisizokuwa za lazima.

Jaji Mwambegele alitoa angalizo kwa mawakala hao kutoka vyama vya siasa kuwa  hawaruhusiwi kuwaingilia watendaji wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao vituoni.

Tume imetangaza uzinduzi wa zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura utafanyika tarehe 01 Julai, 2024 mkoani Kigoma ambapo Mgeni rasmi anataraji kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa na kauli mbiu ya uboreshaji ni  “Kujiandikisha Kuwa Mpiga Kura Ni Msingi Wa Uchaguzi Bora”

No comments:

Post a Comment

Pages