HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 28, 2024

NMB Sabasaba kuhudumia Waoneshaji 3,000, Wananchi 800,000 kwa siku 16

 
Kaimu Meneja wa Kanda ya Dar es Salaam wa Benki ya NMB  Ferdinard Mpona (kushoto) akitoa huduma kwa baadhi ya wateja waliofikia kwenye tawi dogo la NMB lililopo kwenye maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea kuanzia leo hadi tarehe 13 Julai. Benki ya NMB imefungua milango yake kuhudumia wateja na kampuni mbali mbali watakahuduria na kushiriki kwenye maonyesho haya ya Saba Saba.

 

NA MWANDISHI WETU

 

BENKI ya NMB imefungua tawi lake katika Viwanja vya Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba, huku ikiahidi utayari wa kuhudumia kwa ufanisi wateja wake, pamoja na waoneshaji zaidi ya 3,000 wanaoshiriki maonesho hayo na wananchi zaidi ya 800,000 wanaokisiwa kuhudhuria.

 

Maonesho hayo yamefunguliwa rasmi Ijumaa ya Juni 28 na yanatarajia kufungwa Julai 13, ambako tawi hilo na mawakala zaidi ya 35, watatoa huduma kedekede za kifedha, pamoja na Malipo na Tozo za Serikali, Kodi za Mabanda ya Maonesho, Hati za Ardhi, Leseni na TRA kwa siku zote 16.

 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa tawi hilo, Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Ferdinand Mpona, alisema NMB Sabasaba ni tawi kamili litakalohudumia maelfu ya waoneshaji na wahudhuriaji wa maonesho hayo yanayofanyika chini ya kaulimbiu; Tanzania, Mahali sahihi kwa Biashara na Uwekezaji.

 

   “Tuko tayari kuhudumia waoneshaji wote zaidi ya 3,000 na zaidi ya wananchi watakaohudhuria wanaokisiwa kufikia 800,000, wataalamu wetu watakuwa hapa kutoa masuluhishi mbalimbali ya kifedha ikiwemo ufunguzi wa akaunti na huduma zetu Bima, KilimoBiashara na Malipo ya Kodi na Tozo za Serikali.

 

“Tunawakaribisha kufungua akaunti nafuu ya NMB Pesa kwa Sh. 1,000 tu, NMB Kikundi inayojumuisha wana vikundi, NMB Jiwekee maalum kwa akiba ya baadaye, huku pia tukitoa huduma za Malipo ya Kiserrikali, hasa ukizingatia tunaelekea kufunga Mwaka wa Fedha na kufungua mwaka mpya.  

 

“Tunapoelekea kufunga Mwaka wa Fedha wa 2023/24 na kufungua Mwaka Mpya wa 2024/25, kunakuwa na uhitaji mkubwa wa Huduma za Malipo ya Serikali, NMB Sabasaba tunawakaribisha wote kulipia tozo mbalimbali, Hati za Ardhi, Leseni za Biashara na Kodi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),” alisema Mpona.

 

Aliongeza ya kwamba, hakuna haja ya wateja wao na wananchi kutembea na pesa taslimu mkononi kutokea majumbani, badala yake watapata huduma hizo katika Tawi la NMB Sabasaba na mawakala kibao waliotapakaa katika viwanja hivyo kuthibitisha kwa vitendo kaulimbiu ya NMB Karibu Yako.

 

“Aidha, kuna fursa mbalimbali za uwekezaji, kama ambavyo kaulimbiu ya maonesho haya inavyosema; ‘Tanzania Sehemu Bora kwa Biashara na Uwekezaji, kwa hiyo tutakuwa na wataalamu mbalimbali wanaohusika na elimu ya mikopo ya uwekezaji kwa wafanyabiashara na wawekezaji wengine,” alisisitiza Mpona.

 

Katika Viwanja vya Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara, Tawi la NMB Sabasaba linapatikana kwenye Banda namba 24C, lililopo makutano ya mitaa ya Mabalozi na Carnivore, pembezoni mwa Banda la Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Tanzania (SIDO).

 

 

No comments:

Post a Comment

Pages