HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 18, 2024

Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam wazindua Shindano la Teknolojia (U.S. -Tanzania Tech Challenge) la Dola za Kimarekani 250,000

Dar es Salaam, 18 Juni 2024 – Mshauri wa Diplomasia ya Umma wa Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania Jeanne Clark leo katika hafla iliyoandaliwa na AidData/REPOA yenye mada kuu isemayo “Wekeza kwa Watu wa Tanzania” ametangaza kuwa Ubalozi wa Marekani kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani wataendesha shindano la wazi kwa sekta binafsi na/au asasi za kiraia watakaowasilisha maandiko ya miradi yatakayosaidia suluhisho za kibunifu za kukuza ushiriki wa raia, kuimarisha jitihada za kukuza uelewa kuhusu dhima, wajibu na utendaji wa vyombo vya habari (media literacy) na utoaji taarifa sahihi na za kuaminika (information integrity) nchini Tanzania. 

 

Tunawakaribisha wataalamu wa teknolojia na waleta mabadiliko kutoka nchini kote Tanzania kuwasilisha mapendekezo yao na suluhisho kwa hadhira mbalimbali ikiwa ni pamoja na serikali, asasi za kiraia na sekta binafsi. Hadi taasisi zipatazo nane zitachaguliwa kuwasilisha teknolojia zao kwa jopo la majaji. Miongoni mwazo, taasisi tatu zitachaguliwa kuwa washindi wa shindano hili na kupokea ruzuku zenye jumla ya Dola za Kimarekani 250,000. Miradi au suluhisho zitakazoshinda zitatekelezwa kwa manufaa ya Tanzania pekee.

 

Washiriki wanaweza kuwasilisha miradi inayotumia teknolojia za kisasa kutoa suluhisho mbalimbali, iwe ni programu za kielimu, majukwaa ya michezo ya kielektroniki (gaming platforms), zana za kuthibitisha ukweli wa taarifa (fact-checking tools), zana za kuthibitisha mtoa maudhui na maudhui yenyewe (content-authentication tools) na mada nyingine mbalimbali. Ni lazima maandiko ya miradi yalenge katika kukuza uwajibikaji wa raia (civic responsibility) na ushiriki kamilifu wa jamii (community engagement); pamoja na kusaidia kupanua uelewa na matumizi ya rasilimali za kidijitali ikiwemo katika maeneo yasiyofikiwa kirahisi na vyombo vya habari.

 

Shindano la Teknolojia litafanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam, tarehe 18 na 19 Septemba. Siku ya kwanza ya shindano itahusisha maonyesho ambapo wataalamu wa teknolojia au taasisi zitakazokuwa zimechaguliwa zitaonyesha kazi zao;  siku ya pili itahusisha majadiliano ya wanajopo watoa mada (panel discussions) na mijadala itakayowahusisha wataalamu wa teknolojia, maafisa wa serikali, asasi za kiraia, taasisi za elimu na vyombo vya habari ili kujadili mafunzo yatakayokuwa yamejitokeza na fursa za kushirikiana katika  kushughulikia changamoto ya kukuza ushiriki wa raia, kuongeza uelewa kuhusu dhima, wajibu na utendaji wa vyombo vya habari na kuimarisha mazingira ya upashaji habari. Kwa wale watakaopenda kutuma maombi ya kushiriki katika Shindano hili la Teknolojia, wanaweza kupata maelezo zaidi katika tovuti https://cvent.me/Z0Am03

 

Kupitia Shindano la Teknolojia, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani inalenga kusaidia makampuni ya kiteknolojia na/au taasisi za Kitanzania ili kuendeleza jitihada zao za kubuni na kutengeneza suluhisho za kibunifu zinazolenga kuinua ushiriki na uwajibikaji wa raia kwa kukuza uelewa wao kuhusu dhima, wajibu na utendaji wa vyombo vya habari. Aidha, tunaamini katika majadilino yanayojenga kuhusu ushiriki wa raia, kuboresha uelewa kuhusu dhima, wajibu na utendaji wa vyombo vya habari na mazingira imara ya upashaji habari kati ya makampuni ya teknolojia na Kitanzania, taasisi za elimu, mashirika ya vyombo vya habari na wadau wa serikali.

 

Tafadhali zingatia kuwa mtu mmoja mmoja hataruhusiwa kushiriki katika shindano hili. Zawadi kwa washindi wa Shindano la Teknolojia zitatolewa tu kwa mashirika ya sekta binafsi au asasi za kiraia. Waombaji wa ruzuku watatakiwa kujaza kikamilifu fomu maalumu ya maombi kama ilivyoelezwa katika tovuti.

No comments:

Post a Comment

Pages