Na Selemani Msuya
IMEELEZWA iwapo wanawake watapewa elimu ya kuzuia biashara haramu ya viumbe pori au wanyamapori, biashara hiyo itakoma na viumbe hao watakuwa endelevu.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Kitengo cha Sera Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Allen Mgaza wakati akijibu swali la mwandishi wa habari kwenye mdahalo wa asubuhi ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET).
Mdahalo huo ambao umerushwa mbashara kupitia TBC Safaei Chanel, umefadhiliwa Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili ulibeba ajenda ya Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi katika Kutokomeza Biashara Haramu ya Wanyamapori.
Akijibu swali hilo Mgaza amesema vita dhidi ya biashara haramu ya viumbe pori ni jumuishi, hivyo ni lazima wanawake wapewe kipaumbele zaidi katika vita hiyo.
“Mapambano ya biashara haramu ya viumbe pori yanapaswa kuwa jumuishi na kundi la wakina mama ni muhimu sana, nadhani kila mmoja anajua nafasi ya mama nyumbani na kwenye jamii, kwani iwapo baba atashiriki kufanya ujangili na kuleta nyama nyumbani ambaye anaipika ni mama, hivyo mama akielewa hasara zake atakuwa balozi sahihi kuongoza vita hiyo,” amesema.
Mgaza amesema USAID Tuhifadhi Maliasili imehusisha makundi yote katika kutoa elimu ya madhara ya uwindaji haramu wa viumbe pori na wanaanza kuona matokeo chanya.
Mkuu huyo wa kitengo amesema iwapo kila mtetezi wa viumbe pori ataweka mkazo kweenye kutoa elimu hasa kwa wanawake viumbe hao watakuwa salama na endelevu.
“Wanawake ndio chachu ya mabadiliko ya jamii, kwani baba akikamatwa na meno ya tembo, jukumu la kulea watoto litabaki kwa mama, hivyo mama ni mtu muhimu sana katika haya mapambano,” amesisitiza.
Amesema biashara haramu ya viumbepori inafanyika duniani kote ambapo wao kama USAID wanafanya kazi na makundi yote ili kuhakikisha elimu ya kukabiliana na biashara hiyo inafanikiwa.
Mgaza amesema biashara haramu sio mpya, ipo kwa miaka mingi, hivyo kinachohitajika ni kila mwana jamii kuthamini viumbe pori hivyo kwani vinategemeana.
“Biashara ya viumbe pori ipo na inaruhusiwa kufanyika, lakini ina taratibu zake, lazima iwe halali inayofuata sheria za nchi na za kimataifa na kuwa endelevu, kwa maana kwamba hatutaki biashara ifanyike kwa njia haramu na kumaliza rasilimali zetu zote na vizazi vijavyo vikose,” amesema.
Amesema biashara hiyo inatakiwa kunufaisha wananchi wakiwemo wanawake ambao kwa asilimia kubwa wanakuwa wahanga wa matukio ya biashara haramu ya viumbe pori.
Aidha amesema taarifa zinaonesha kuwa watu wanaofanya biashara haramu ya viumbepori wamekuwa wakitumia fedha hizo kufanya mambo mengi ambayo hayakubaliki kwenye jamii na dunia.
Pia mtaalam huyo amesema biashara haramu kwa ngazi ya dunia inaonesha viumbe pori vya nchi kavu na majini vinahusika katika biashara hiyo, hivyo juhudi zinahitajika katika maeneo hayo ili wanyama hao wawe salama na endelevu.
Mwenyekiti wa Baraza la Wasafirishaji Shehena Tanzania (TSC), Clement Kamendu amesema wanaunga mkono dhana nzima ya ushirikishwaji kwani ndio ngao muhimu ya kukabiliana na janga hilo la dunia.
Amesema baraza lao lina jukumu la kulinda maslahi ya wasafirishaji wa shehena kwenda nje na kuingiza nchini, hivyo watashirikiana na kila mtu kuzuia biashara haramu ya viumbe pori.
Mwenyekiti huyo amesema wanatoa elimu kwa wadau wote ambao wapo kwenye mnyororo huo, ili kuepukana na biashara hiyo.
Kamendu amesema usafirishaji viumbepori kwa njia halali unachangia asilimia tisa ya pato la taifa na fedha za kigeni asilimia 25, hivyo ni wazi sekta hii ina faida iwapo itasimamia vema.
“Kipindi cha 2009 hadi 2018 ripoti ya serikali ilionesha shehena 15 zilikamatwa na watu 1,072 walihusika na kusababisha kesi za jinai 391 kufunguliwa, watu 301 kufungwa, 43 walipigwa faini ya Sh bilioni 1.5 na wahusika kufungwa miaka 3,015,” amesema.
Amesema kuanzia 2009 hadi 2015 zilikamatwa shehena 23 za meno ya tembo ambazo zilipitia Bandari ya Dar es Salaam na Zanzibar na hayo yote yalichangiwa na dhana nzima ya ushirikishwaji.
Amesema takwimu zinaonesha kwa mwaka duniani tani bilioni 12 zinasafirishwa na Afrika ikihusika na asilimia 6 ya bidhaa hizo ambapo katika hizo zipo shehena haramu.
“Asilimia 80 ya bidhaa zinazosafirishwa duniani kibiashara kwa uzito zinatumia njia ya bahari na asilimia 70 kwa thamani pia zinatumia njia hiyo hiyo, hivyo sekta ya usafirishaji ikielewa ukubwa wa tatizo itaweza kusaidia serikali katika mapambano,” amesema.
Kamendu amesema wamekuwa wakitoa elimu kwa wasafirishaji wote wakiwemo wa mabasi, ndege, meli na wengine, jambo ambalo limekuwa na matokeo chanya.
Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo amesema wameweka kwenye kutoa elimu kwa wahariri na waandishi wa habari ili waweze kuelezea sekta hiyo kwa usahihi.
Amesema biashara hiyo haramu ya viumbe pori au wanyamapori isipopigwa vita miaka michache jamii itakuwa inahadithiwa kuhusu viumbe hivyo na kwamba kalamu za waandishi zinaweza kuifanya Tanzania na dunia kuwa salama zaidi.
“JET kwa kushirikiana na USAID Tuhifadhi Maliasili, imeamua kutoa mafunzo kwa wanachama wake ili wawe na uelewa biashara haramu za viumbe pori na masuala ya uhifadhi tunaamini kupitia kalamu zao hali itakuwa nzuri,” amesema.
June 21, 2024
Home
Unlabelled
Wanawake nyenzo ya kuzuia biashara haramu ya viumbe pori
Wanawake nyenzo ya kuzuia biashara haramu ya viumbe pori
Share This
About HABARI MSETO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Author Details
Ut wisi enim ad minim veniam, quis nostrud exerci tation ullamcorper suscipit lobortis nisl ut aliquip ex ea commodo consequat. Duis autem vel eum iriure dolor in hendrerit in vulputate velit esse molestie consequat.
No comments:
Post a Comment