HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 05, 2024

DL Group yajipanga kulipa wafanyakazi ndani siku saba

Na Mwandishi Wetu, Njombe

MWEKEZAJI wa viwanda na mashamba ya Chai yaliyopo Mkoani Iringa na Njombe amesema Kampuni ya DL Group ipo mbioni kulipa mishahara ya miezi miwili kwa wafanyakazi wake wote viwandani na mashambani ndani ya siku saba kuanzia leo.

Akizunzungumza na  waandishi wa habari leo, miongoni mwa wakurugezi wa Kampuni ya DL Group inayomiliki viwanda vya kuchakata chai vya Itona, Kibena, Ikanga na Luponde Bw Colins Otieno amesema kuporomoka kwa soko la chai duniani na kuadimika kwa dola kumechangia ucheleweshwaji wa malipo ya mishahara kwa wafanyakazi.

“Soko la chai Afrika Mashariki limezidi kudorora kutokana na vita vinavyoendelea kati ya Ukraine na  Urusi, Israel na Palestina ambapo mataifa hayo nimiongoni mwa wanunuzi wakubwa wa chai inayozalishwa Afrika Mashariki ikiwemo nchi ya Tanzania,” alisema Otieno na kuongeza kuwa  kuadimika kwa dola kumechochea kushuka kwa soko la chai duniani.

Amesema wamekuwa wakipata   dola ya Kimarekani 0.6 kwa kilo kwenye mapato ya hisa ya chai ambayo haiendani na gharama wanayoitumia kwenye uzalishaji na hivyo imechangia kwa kiasi kikubwa kampuni kushindwa kulipa mishahara kwa wakati na kwamba wapo katika hatua za mwisho za kupata utatuzi

“DL Group imejipanga kufanya kazi na serikali na vilevile tunatambua mchango wa Waziri wake wa Kilimo, Hussein Bashe, Mkuu wa Mkoa wa Njombe Anthony Mtaka na Bodi ya Chai Tanzania,” alisema Otieno na kuongeza kuwa kampuni yake inaendelea na mazungumzo na serikali   kuona namna itakavyo wajengea uwezo wakulima wadogo wadogo na wafanyakazi wake ili kuinua sekta ya chai nchini.

Otieno  amesema DL Group  kwa kushirikiana na serikali wanakusudia kuboresha maisha ya wakulima wadogo wadogo,  ambapo  itanarajia kuiuzia serikali mashamba yake matatu ili kuwapa wakulima wadogo  ambao ni miongoni mwa  wale watakao nufaika na mafunzo yatakayo tolewa na kampuni ya   Kenya Tanzania Development Authority (KTDA)

 “Tupo kwenye mazungumzo na kampuni ya   Kenya Tanzania Development Authority (KTDA ambayo ina viwanda 70 na wakulima zaidi ya laki saba (700,000) hivyo wakulima wadogo wadogo watajengewa uwezo wakuzalisha zaidi na kuwa na soko la uhakika,” alisema

Otieno amepongeza hatua mbalimbali  zinazochukuliwa na  serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk Samia Suluhu Hassani katika kuendeleza sekta ya kilimo ambayo inamchango mkubwa katika kukuza sekta ya utalii hapa nchini.

Amesema kuyumba kwa soko la chai sio Tanzania pekee bali ni  Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla hivyo kuwata wanasiasa wasitumie changamoto hiyo kujinufaisha kisiasa.

Naye Michael  Mwenda ambaye ni mafanyakazi wa kiwanda cha Kibena akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wenzake,  amempongeza  muwekezaji wa kiwanda kwa  kuchukua hatua madhubuti na kuwahakikishia wafanyakazi kulipwa stahiki zao ndani ya kipindi cha siku kumi.

“Pamoja na matatizo mbalimbali yanayoikabili sekta ya chai, DL Group imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha inaboresha maslahi ya wafanyakazi. hiki kilichotokea hapa katikati ni kitu ambacho atukutarajia lakini huko mbele dalili ni njema,” amesema Mwenda.

Kampuni   ya  DL Group  mpaka sasa hivi ishawekeza zaidi ya Sh bilioni 25 inamiliki mashamba tisa katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Iringa na Njombe  sambamba na kumiliki viwanda vya kuchakata chai  cha Itona kilichopo  Mufindi, kiwanda cha Kibena (Njombe) na Ikanga ( Lupembe)



No comments:

Post a Comment

Pages