Makamu Mwenyekiti Wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe. Mbarouk Salim Mbarouk akizungumza wakati akifungua mkutano wa siku moja wa Tume na Wadau wa Uchaguzi uliofanyika leo Julai 24, 2024 Mjini Bukoba Mkoani Kagera.Wadau hao ni
pamoja na Viongozi wa vyama vya siasa,
Viongozi wa Dini, Wawakilishi wa Asasi za Kiraia, Wahariri wa Vyombo vya
habari, Waandishi wa habari, Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri,
Wawakilishi wa Makundi mbalimbali ya Vijana, Watu wenye
ulemavu, Wanawake na Wazee wa Kimila.
*******************
Na. Waandishi Wetu, Geita na
Kagera
Uboreshaji wa Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura mkoani Geita na Kagera utafanyika kwa siku saba kuanzia
tarehe 05 hadi 11 Agosti, 2024 ambapo vituo vitafunguliwa saa 2:00 asubuhi na
kufungwa saa 12:00 jioni.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele wakati akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi mkoani Geita leo tarehe 24 Julai, 2024.
Mkutano kama huo mkoani Kagera
umefunguliwa na Makamu Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Juji Rufaa (Mstaafu) Mbarouk
Salim Mbarouk. Mikutano hiyo inafanyika ikiwa ni maandalizi ya uboreshaji wa
Daftari kwenye mikoa hiyo.
“Mzunguko wa pili wa
uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utajumuisha mkoa huu wa Geita na
Kagera ambapo uboreshaji utaanza tarehe 5 hadi 11 Agosti, 2024. Vituo
vitafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni,” amesema
Jaji Mwambegele.
Ameongeza kuwa mikoa hiyo
inafanya uboreshaji kwenye mzunguko wa pili baada ya mzunguko wa kwanza ambao
umejumuisha mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora ambako uboreshaji umeanza tarehe
20 Julai, 2024 na unatarajiwa kukamilika tarehe 26 Julai, 2024.
“Tume tayari imeanza zoezi la
uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambapo uzinduzi ulifanyika
mkoani Kigoma tarehe 20 Julai, 2024 na mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB). Uzinduzi
huo umeenda sambamba na kuanza kwa mzunguko wa kwanza wa uboreshaji kwenye
mikoa mitatu ya Kigoma, Tabora na Katavi. Uboreshaji wa Daftari kwenye mikoa
hiyo unaendelea hadi tarehe 26 Julai, 2024,” amesema.
Akizungumza mkoani Kagera,
Mhe. Jaji Mbarouk amesisitiza kuwa kadi za wapiga kura zilizotolewa mwaka 2015
na 2020 ni halali na zitaendelea kutumika kwenye chaguzi zijazo. Hivyo,
amewataka wadau wa uchaguzi kwenye mkoa huo kuwaelimisha wapiga kura wenye kadi
hizo wasiende kuboresha taarifa zao kwa kuwa zoezi hilo haliwahusu.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 168
cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024 kadi za
mpiga kura zilizotolewa mwaka 2015 na 2020 zenye jina la Tume ya Taifa ya
Uchaguzi ni halali na zitaendelea kutumika kwenye chaguzi zijazo. Hivyo, zoezi
hili la uboreshaji wa Daftari haliwahusu wapiga kura wenye kadi hizo,” Jaji
Mbarouk amesema.
Akizungumzia teknolojia ya
uandikishaji wa wapiga kura wakati wa kuwasilisha mada, Mkurugenzi wa Uchaguzi
wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhan amesisitiza kuwa wapiga
kura wanaoboresha taarifa zao wanaweza kuanza mchakato wa awali kwa kutumia
simu janja au kiswaswa na kompyuta kupitia mfumo ujulikanao kama Online Voters
Registration System (OVRS) au kwa kubobya *152*00#, kisha namba 9 na kufuata
maelekezo.
”Mtumiaji wa huduma hii,
atatakiwa kufika kituo anachokusudia kujiandikisha ili akamilishe hatua za
kupigwa picha, kuweka saini na kupatiwa kadi yake ya mpiga kura,” amesema Bw.
Kailima.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele wakati akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi mkoani Geita leo tarehe 24 Julai, 2024.
No comments:
Post a Comment