HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 07, 2024

KIBAHA TC YAFANYA KWELI YAVISAIDIA VITUO TISA VYA KULELEA WATOTO YATIMA

NA VICTOR MASANGU, KIBAHA

Halmashauri ya mji Kibaha katika kuunga mkono juhudi za Rais wa awamu ya sita Dkt.Samia Suluhu Hassan kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalumu imetoa msaada wa mahitaji mbali kwa vituo tisa ambavyo vinalea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.

Msaada huo ambao  umetolewa leo na kukabidhiwa kwa viongozi wa vituo uliambata na halfa ya kula chakula  cha pamoja kati ya watoto hao pamoja na viongozi mbali mbali wa serikali,viongozi wa chama pamoja na viongozi wa dini.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Kibaha mji Rogers Shemwelekwa  akikabidhi msaada wa mahitaji hayo kwa viongozi wa vituo hivyo  amesema kwamba wameamua kufanya hivyo kwa lengo la kuweza kuwasaidia kwa pamoja watoto mahitaji mbali mbali ambayo itakuwa ni muhimu katika mazingira wanayoishi.

Mkurugenzi huyo alibainisha kwamba misaada ambayo imetolewa ni zaidi ya mahitaji 19 ambayo yamegharimu kiasi cha  zaidi ya shilingi milioni  40.

"Sisi kama Halmashauri tumeamua kuvisaidia vituo hivi tisa vya watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu lakini pia jambo ili tumeweza kushirikiana na wadau wa maendeleo ikiwemo shirika la elimu kibaha,benki ya CRDB pamoja na wadau wa maendeleo,"alisema Mkurugenzi.

Mkurugenzi alivitaja vituo hivyo ni  Shaloom,Buloma Foundation,Sifa Foundation, Fadhila Faundation,Madina,Haven of Peace,Kibaha Children,pamoja na Karibu nyumbani.

Kadhalika Mkurugenzi huyo alivitaja baadhi ya misaada ambayo wameitoa ni pamoja na magodoro,mafuta ya kula,miswaki,pipi,sabuni za unga,stamina kwa ajili ya watoto,dawa ya miswaki,pamoja na vifaa mbali mbali vya mashuleni.

Aidha mkurugenzi huyo katika hatua nyingine aliwashukuru kwa dhati wadau wa maendeleo ambao wameweza kujitokeza na kuweza kusaidia  kuwachangia kwa hali na mali mahitaji  mbali mbali.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri yaKibaha mji Mussa Ndomba amesema kwamba lengo ni kuweka mipango madhubuti ya kuwasaidia watoto ambao wanaishi katika mazingira magumu pamoja yatima.

Ndomba alibainisha kuwa wataendelea kushirikiana na wadau mbali mbali wa maendeleo ili kuhakikisha wanaendelea kusapoti vituo vyote ambavyo vinalea watoto wenye mahitaji maalumu.

Pia Ndomba aliongeza kuwa pia Halmashauri itaendelea kupambana katika kutatua kero na changamoto za wananchi ili kuwaletea maendeleo.

Naye Afisa ustawi wa Jamii katika halmashauri ya mji Kibaha  Faustina Kayomba alisema kwamba katika vituo hivyo tisa kuna jumla ya watoto wapatao 601 ambao wengi wao ni watoto yatima na wengine wanaoishi katika mazingira magumu.

Alibainisha kwamba watoto hao wamekuwa wanakutana na changamoto mbali mbali ikiwemo kuwepo kwa mahusiano mabaya ya wazazi na walezi wao.

Nao baadhi ya viongozi kutoka vituo hivyo vilivyopatiwa msaada walimpongeza Mkurugenzi wa halmashauri ya mji Kibaha  pamoja na timu yake kwa kuona umuhimu wa kutoa wazo hilo la kuwasaidia mahitaji mbali mbali kwa ajili ya watoto hao.

Baadhi ya watoto wanaolelewa katika vituo hivyo wametoa pongezi na shukrani kwa uongozi wa halmashauri ya Kibaha mji pamoja na wadau wengine wa maendeleo kwa kuwasaidia mahitaji yao muhimu.


 

No comments:

Post a Comment

Pages