Na Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Viti Maalum (CHADEMA), Sophia Mwakagenda amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuunga mkono kampeni yake ya kuchangia fedha kwa ajili ya kuwapatia bima ya afya zaidi ya watu 2,000 kutoka familia masikini nchini.
Mwakagenda ametoa ombi hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mapambano ya hisani yanayotarajiwa kufanyika mkoani Geita Julai 28 mwaka huu.
Mapambano hayo yatashirikisha mabondia marufu Karim Mandonga, Mada Maugo, Ibrahim Class na wengine ambapo fedha zitakazopatikana zitatumika kulipia bima ya afya kwa watu 2,000 wanaotoka familia masikini.
Mbunge huyo amesema kampeni hiyo inaenda kugusa jamii ya Kitanzania, hivyo anamuomba Rais Samia kumuunga mkono kwa kulipia bima za Watanzania 300 wanaishi katika umaskini.
“Pamoja na Rais Samia, pia namuomba Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko, Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson, Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma, taasisi za umma na binafsi kuniunga mkono katika kampeni hii muhimu kwa jamii ya Kitanzania.
Amesema fedha ambazo zitapatikana zitakabidhiwa na Mfuko Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) ambayo inatambua kaya maskini nchini kote.
Mwakagenda amesema kwa anavyomfuatilia Rais Samia na wasaidizi wake ana imani watachangia kampeni hiyo ili kuwezesha Watanzania wengi kupata bima ya afya.
Amasema Taasisi yake ya Lady in Red imejipanga kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali kuhakikisha inatatua changamoto ya bima kwa wananchi hasa maskini.
Mkurugenzi huyo wa Lady in Red amesema yeye ameamua kuwapa mabondia kipaumbele na ndio maana kila akifikiria kufanikisha jambo la hisani kundi hilo ndio la kwanza.
“Julai 28 tukutane Geita ambapo Mandonga anatarajia kupanda ulingoni kulipiza kisasi kwa Mada, lakini pia kwa mara ya kwanza Ibrahim Class ataonesha umwamba wake Geita na wengi ila yote hayo ni kuniunga mkono katika kusaidia jamii inayoishi kwenye umasikini,” amesema.
Mwakagenda amesema Mandonga na Mada watapigana kwa raundi sita huku Class akipambana kwa raundi 10.
Aidha, amesema Bondia Mkongwe, Japhet Kasseba anatarajiwa kupanda ulingoni, hivyo kuwataka wananchi wa Geita na mikoa ya jirani wasithubutu kukosa.
Mbunge huyo amesema kinachoenda kupatikana Geita kinaenda kufasiri bima za afya kwa wote, hivyo anaomba kila mwenye uwezo kujitolea ili kufanikisha.
Amesema ngumi hizo za hisani katika kuchangia bima ya afya zitanufaisha mikoani Geita, Dodoma, Mbeya, na Pwani ikiwa ni kuendelea mpango wao ulioanza mwaka 2016 kusaidia jamii.
Mbunge huyo amesema pia siku hiyo kutakuwa na mapambano ya wabunge mbalimbali akiwemo Mbunge wa Geita Constantine Kanyasu dhidi Vuma Augustino wa Kasulu Vijijini, Stanslaus Mabula wa Nyamagana dhidi Seif Gulamali wa Manonga.
Wabunge wengine watakaopambana ni Santiel Kilumba na Sylivia Sigula, Salome Makamba na Ngwasi Kamani wote wa viti maalum.
Akizungumzia pambano hilo la hisani Bondia Mandonga amesema amefurahi kuwa sehemu ya mabondi ambao watashiriki kusaidia kaya masikini ambapo ameahidi kumpiga Maugo kwa ngumi inayoitwa ‘Mbeku’.
“Baada ya Maugo kukimbia ghetto Morogoro, sasa naenda Geita kumpiga kwa ngumi inayoitwa ‘Mbeku’ ambayo ilihusika kuleta Uhuru wa Tanzania. Mada Maugo atake tunampiga, asitake tunampiga. Ila kusema kweli nimefurahi sana kushiriki pambano hili la hisani, naomba waheshiwa wengine waunge mkono juhudi,” amesema.
Kwa upande wake, Maugo alisema safari hii itakuwa mwisho kwa Mandonga kucheza ngumi, kwani amepanga kumpiga aina ya ngumi iitwayo 'Pikitieli'.
Naye bondia Ibrahim Class amesema amepata faraja kushirikishwa katika pambano hilo la hisani na kuahidi kuonesha mchezo mzuri kwani mikono inawasha.
Bondia Kaseba amesema juhudi anazofanya Mbunge Mwakagenda zinapaswa kuungwa mkono na wapenda maendeleo wote, ili kuweza kusaidia jamii ya Tanzania.
July 04, 2024
Share This
About HABARI MSETO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Author Details
Ut wisi enim ad minim veniam, quis nostrud exerci tation ullamcorper suscipit lobortis nisl ut aliquip ex ea commodo consequat. Duis autem vel eum iriure dolor in hendrerit in vulputate velit esse molestie consequat.
No comments:
Post a Comment