HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 23, 2024

Miundombinu maghorofa ya Magomeni Kota yaibua vilio, TBA lawamani

NA MWANDISI WETU

VILIO vya miundombinu mibovu katika maghorofa ya Magomeni Kota, vimeendelea kutolewa na wakazi wa majengo hayo, ambao wameitupia lawama Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), wakilaumiwa kwa ujenzi usio na viwango vinavyolingana na ukubwa, uwingi wa watu na mahitaji yao.

Mradi huo uliojengwa na TBA, unahusisha maghorofa Matano yaliyozinduliwa Machi 23, 2022 na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, lakini kwa nyakati tofauti kumekuwa na vilio vitokanavyo na kero mbalimbali ambazo msingi wake ni ujenzi unaotajwa na wakazi hao kuwa usio na viwango.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, ametembelea wakazi wa maeneo hayo kusikiliza kero zao, ambako Bi. Mwajuma Khamis kwa niaba ya wakazi zaidi ya 1,200 alimueleza changamoto na kero wanazokabiliana nazo, hasa ubovu wa miundombinu ya majisafi na majitaka.

Akishangiliwa na wakazi hao, Bi. Mwajuma alisema TBA wanastahili kubeba lawama zote zitokanazo na mtanziko wa miundombinu ya majisafi, uondoshaji majitaka, lakini pia kubomoka, kuchakaa na kuharibika kwa majengo hayo haraka kutokana na ujenzi mbovu.


Bi. Mwajuma alisema ingawa kwa sasa hawana deni lolote la Mamlaka ya Maji ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASCO), lakini hawako tayari kuletewa huduma ya majisafi katika maghorofa hayo hadi kutapofanyika marekebisho ya miundombinu yake.

“Hatutaki maji ya Dawasco kwa sababu, maghorofa yote matano yanatumia mita moja inayosambaza majisafi, hii inasababisha wengine kutumia maji bila kulipia. Tumeshamaliza deni la Dawasco, lakini haturuhusu majisafi yaje kwa sababu itazalisha deni jipya kwa kuwa tutatumia kwa fujo.

“Tuko tayari kuruhusu maji ya Dawasco, ila iwe kila kaya na mita yake kama zilivyo mita za umeme, kila kaya ilipie bili yake, lakini Mwenyekiti wa Kamati, (George Cassian) akajibu wakija Dawasco watalazimika kuvunja baadhi ya miundombinu.

“Lakini pia akasema tutalazimika kulipia ufungaji mita kwa kila mtu, sisi tukalikataa hilo kwa sababu, makosa ya kiunganishaji maji hapa yalifanywa na Dawasco wenyewe na TBA waliojenga,” alisema Bi. Mwajuma.

Alibainisha ya kwamba maghorofa hayana ubora kutokana na ukweli makaro ya majitaka hayaendani na ukubwa na uwingi wa wakazi wake; “TBA wametufanyia ujenzi usio na viwango, wametuchimbia makaro, madogo wakati majengo ni makubwa yanayochukua watu wengi.

“Kwa aina ya ukubwa wa majengo haya na uwingi wa wakazi tunaoishi, miundombinu ya majitaka ilipaswa kuelekezwa baharini moja kwa moja, sio kuchimba makaro madogo yanayoruhusu majitaka kukaa humu ndani na kutegemea magari ya kunyonya,” alisisitiza Bi. Mwajuma.

Kwa upande wake, DC Mtambule alikiri uwepo wa changamoto zote zinazolalamikiwa na wananchi, lakini akabainisha ya kuwa iwapo wakazi wa maghorifa hayo wangelipia ‘service charge’ bila kusukumwa, kusingekuwa na kero hizo ndani ya miaka mitano ya wao kuishi bure hapo kabla ya kuuziwa.

“Niko hapa kusikiliza changamoto za awananchi, hapa kuna maghorofa matano yenye kaya 644, ambao wanakibiliwa na tatizo kubwa la maji litokanalo na miundombinu ya majisafi, ambapo kuna pampu mbili tu kwa maana ya zile mita zilizopo chini.

“Hii imeleta shida ambayo pia imetokana na wakazi hapa kutolipia huduma yaani ‘service charge’ kwa sababu hiyo ndio inayotumika kulipia bili za maji, umeme, usafi, ulinzi na huduma nyingine zinazopatikana katika eneo hili.

“Mkwamo huo umesababisha maji kukatwa hapa na sasa wanatumia maji ya visima, huku huduma za ulinzi kuzorota, Nimewaambia wakazi wa hapa zaidi ya 1,200, kwamba ili kupata huduma zote nilizozitaja hapo, kila mkazi anapaswa kulipia ‘service charge’ kwa wakati.

“Na lazima kamati husika itoe taarifa za mapato na matumizi ya pesa hizo kwa wakazi wa hapa mara kwa mara,” alisisitiza DC Mtambule ambaye alifafanua kuwa kulipia ‘service charge’ kutaleta huduma bora za ulinzi, usafi, maji, umeme na mengineyo ndani ya miaka mitano ya kukaa bure iliyotolewa na Rais Samia.

Aliongeza ya kuna wakazi wa maghorofa hayo ambao hawajasaini mikataba kama inavyotakiwa, huku akiishukuru Serikali iliyoelekeza wakazi wakae miaka mitano bure katika majengo hayo, lakini baada ya hapo, ndani ya miaka 25 walipie manunuzi ya nyumba hizo kiasi cha Sh. Milioni 48.

“Nimewaambia ili kutimiza matakwa ya kisheria ya kuwepo hapa, wanapaswa kusaini mikataba, nimewaagiza TBA kushirikiana na wakazi hapa kupitia upya mchakato huo kwa mara ya mwisho, kuwapa ufafanuzi wananchi hapa na kusaini mikataba na kutambulika kisheria,” alisema DC Mtambule.




No comments:

Post a Comment

Pages