NA MWANDISHI WETU
KUELEKEA Kikao Kazi cha Ofisi ya Msajili wa Hazina na Maofisa Watendaji Wakuu, Wakurugenzi na Wenyeviti wa Bodi wa Taasisi za Umma, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, amebainisha kwamba dhima kuu itakuwa dhana moja muhimu ya kuimarisha utendaji kazi wa Makampuni ya Tanzania nje ya mipaka yetu.
Kikao Kazi hicho siku tatu kinachotarajiwa kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 600, kitafanyika katikati ya mwezi ujao jijijni Arusha, ambako Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anatarajia kuwa mgeni rasmi, kuangalia utekelezaji wa maagizo yake aliyoyatoa mwaka jana aliposhiriki kikao kazi cha kwanza kama hicho.
Akizungumza na wahariri na waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Salaam, Mchechu alisema dhima ya kuangalia uwekezaji na utoaji huduma wa taasisi za ndani nje ya mipaka, itaanza na taasisi zenye utayari, hususani zile zilizopata mafanikio ndani ya nchi.
“Rais Samia alikubali kuwa mgeni rasmi, kama tulivyomuomba Siku ya Gawio na sasa atashiriki kikao hiki kitachojumuisha Maafisa Watendaji Wakuu, Wakurugenzi na Wenyeviti wa Bodi zaidi ya 600, ambacho kitajielekeza katika kuona makampuni ya Tanzania yanavyoimarisha shughuli zake nje ya mipaka yetu.
“Kwa sababu haya yalikuwa ni maagizo na changamoto kutoka kwa Mheshimiwa Rais Samia mwenyewe aliyokuwa ametupatia katika kikao cha kwanza kama hiki mwaka jana.
“Katika dhima hii ya kutaka kuwa na uwekezaji wa taasisi za umma nje ya nchi, lengo letu ni kuanza na taasisi zenye utayari wa kuvuka mipaka ya nchi, huku lengo la pili likiwa ni kuzifanya taasisi zijue kwamba zinapaswa kubadilika, lakini zifanye hivyo zikiwa na taswira kubwa wanayoiona mbele.
“Kwa hiyo ni wazi lazima watakuwa ni wale wanaofanya vizuri ndani ya nchi, ndio wataweza kwa urahisi kwenda nje ya nchi. Tunaposema kwenda nje ya nchi, haimaanishi tu kwenda kuwekeza mitaji kule, tunalenga pia kufikisha huko huduma zitolewazo ndani ya nchi,” aliongeza.
Akitolea mfano mashirika kama ATCL, alisema ingawa inatambulika kwamba huduma zake zinapatikana nje ya nchi, lakini ofisi yake inadhani kwamba zinapaswa ziende nje na kugusa jamii ya huko kwa ufanisi na ushindani mkubwa.
“Mfano wa pili ni Kampuni kama TRC na Tazara, ni kampuni ambazo ili zifanye vizuri katika huduma zake ni lazima ziguse usafirishaji unaovuka mipaka ya nchi yetu na kwa kufanya hivyo, tutaweza kupata ‘rertuns’ kama nchi, je tunaweza kupata maslahi ya kile tulichokiwekeza huko.
“Kwa hiyo tunapozungumza ‘investment beyonds Tanzania,’ ni kuangalia nini tunaenda kufanya nje. Lakini zipo nyingine zinazoweza kwenda kufanya uwekezaji kabisa nje ya nchi,
tunatamani mabenki yetu makubwa yawe na uwekezaji mkubwa nje ya mipaka yetu, wawe na matawi yao nje ya Tanzania.
“Tuna Benki ya CRDB ambayo wako Burundi na sasa wanaenda DRC, lakini tunamani CRDB au NMB wanakuwa na uwekezaji mwingi zaidi nje ya nchi, kwa sababu tayari washakua wakubwa ndani ya nchi yetu,” alisisitiza Mchechu katika mkutano huo na wahariri na kuongeza:
“Sasa maana yake ni nini? NMB leo hata wakiwa na tawi Zambia, kukiwa na wafanyabiashara wanaoendesha shughuli zao katika kikoa ya Mtwara au Lindi, hawatoumiza kichwa namna ya kufanya miamala ya kibiashara katika nchi za Zambia au Malawi, kwa sababu tayari ana benki ambayo ina matawi ndani ya nchi na nje.”
Mchechu alisema ndio maana Wakenya, wananufaika na uwepo wa matawi ya benki zao za KCB na Equity ambazo zipo nchini Tanzania, hivyo ni rahisi sana kwa Mkenya kufanya biashara kwa ufanisi nchini, na kwamba Tanzania nayo inapaswa kuwa mahiri, lakini ianze katika ngazi hizo.
Aliongeza kuwa, pamoja na hayo kikao hicho kina umuhimu mkubwa, ikiwemo kujua maagizo na maelekezo ya Serikali kupitia viongozi wakuu ya wapi wanataka tuelekee na kwa kasi gani, ikiwa ni pamoja na maafisa watendaji wakuu na wenyeviti wa bodi kubadilishana mawazo na mbinu mbalimbali za uendeshaji biashara.
Aidha, Mchezo aliwaleza wanahabari hao kuwa, katika dhima nne (4R’s) alizokuwanazo Rais Samia, Ofisi ya Msajili imechukua R mbili za ‘Reforms na Rebulding’ ambazo wataendelea kuzisimamia hizo na kwamba mabadiliko ya utendaji wa taasisi ni safari ndefu, na sio jambo la siku mmoja, mwaka mmoja wala sio la taasisi moja.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, alisema agizo la Rais Samia kutaka taasisi, mashirika na makampuni yetu kuvuka mipaka ya nchi katika kuhudumia, liliwahi kutolewa na aliyekuwa Rais wa Kwanza, Hayati Julius Nyerere, akiumizwa na ukubwa wa taasisi zetu kwa ndani tu.
“Mwalimu Nyerere aliwahi kuonesha kuumizwa na uwekezaji wa Benki ya NMB, aliwahi kusema na namnukuu; ‘Tunaposema hizi ni benki kubwa kubwa, hivi ni vibenki viko katika nchi zetu tu Tanzania hapa, hatuzioni zikitoa huduma nje ya nchi huko, zina ukubwa gani..’
“Leo Rais wa Awamu ya Sita Dk. Samia anazungumza kile ambacho Rais wa Awamu ya Kwanza alikizungumza miaka ya 1990 huko na kuweka mikakati ya kuvuka nje. Tumeona NBC wamefanya, tumeona NMB nao wamefanya kubwa.
“Msajili wa Hazina, pamoja na uwekezaji nje, nadhani mnapaswa kufanya kitu kuelimisha Watanzania juu ya kilichofanywa na NMB katika Soko la Hisa la London. Uwekezaji wa nje wa mitaji na kufungua matawi, nimeuliza hapo juu ya nchi zilizoainishwa, nikaambiwa ni nchi za SADC.
“Nadhani kuna haja ya kufikiri na kutafakari kuwekeza mitaji kwa maana ya hisa katika masoko makubwa ya kimataifa ya hisa kwa makampuni na mashirika yetu yanayofanya vizuri, nadhani pengine tutakuwa tumepiga hatua sahihi,” alichangia Kibanda ambaye ni mwenyekiti wa zamani TEF.
No comments:
Post a Comment