HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 11, 2024

Andaeni majina ya watoto kabla ya kuzaliwa wapatiwe vyeti mapema,Waziri Chana

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAZIRI wa Katiba na Sheria Balozi Dkt. Pindi Chana amewataka wazazi kujenga utaratibu wa kuandaa majina ya watoto wao  mapema kabla ya kuzaliwa ili kwa haraka waweze kusajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa mara baada ya kuzaliwa.

 Dkt. Chana ametoa wito huo  mwa wiki  Jijini Dodoma  wakati wa ziara yake ya kujionea  zoezi la usajili  linavyoendela sambamba na  kuwapatia vyeti vya kuzaliwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano katika hospitali ya St.Gemma, kituo cha afya Makole na Zahanati ya Kikuyu zilizopo  Jijini hapa.

 “Leo nimetoa vyeti vya kuzaliwa kwa baadhi ya wakina mama waliojifungua salama na kuruhusiwa nyumbani,”alisema Dkt Chana.

“Nawaomba wazazi  kujenga utaratibu wa kuandaa  jina la mtoto mapema  kabla ya kuzaliwa ili asajiliwe mara baada ya kuzaliwa  na kupatiwa cheti kwani ni haki  ya kila Mtanzania,” alisisitiza  Dkt Chana.

 

Aidha, Balozi Chana amezitaka taasisi mbalimbali za umma na binafsi kuvipokea vyeti hivyo vinavyojazwa  kwa mkono na kutolewa kwa wototo wa umri chini ya miaka mitano wanaosajiliwa katika Ofisi za Watendaji Kata na vituo vya Tiba kote nchini kwani ni vyeti halali na vina hadhi sawa na vyeti vinavyotolewa kwa njia ya compyuta.

“Nitoe rai kwa taasisi mbalimbali za umma na binafsi ambao huvipokea kwa ajili ya kuwapatia wananchi huduma,”alisema na kusisitiza umuhimu wa vyeti vya kuzaliwa kwa kila mtanzania.

 Aidha ,Dkt  Chana amewataka wananchi kuchangamkia huduma hiyo inayotolewa bure nchi nzima, akisema kuwa  vina mchango mkubwa katika kupata huduma mbalimbali, ikiwemo matibabu kupitia bima ya afya, elimu na baadaye ajira na kuzitaka taasisi mbalimbali za umma na binafsi kuvipokea vyeti hivyo kwa ajili ya kuwapatia wananchi huduma.

 “Nipende kuipongeza RITA kwa kazi kubwa wanayoifanya ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Watanzania wanapata vyeti vyao vya kuzaliwa na hili nimejiridhisha pasina shaka kazi hii kubwa ikiendelea kwa ufanisi mkubwa,” alisema.

 Naye Dkt. Flora Mwakalago ambaye ni Kaimu Mganga Mfawidhi wa kituo cha afya cha  Makole, alisema wakati  akielezea mafanikio ya kituo hicho toka kuanzishwa kwa  huduma za  usajili wa vizazi kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano (5) mwaka 2019 kuwa  zaidi ya watoto wachanga 550- 600 huzaliwa kila mwezi huku kati yao  watoto 200- 250 wakipatiwa vyeti vya kuzaliwa.

 “ Kwa kipindi cha  mwezi julai, 2023 hadi  kufikia juni, 2024 tayari  tumeshasajili na kuwapa vyeti vya kuzaliwa watoto zaidi ya  2,750 haya ni matokeo mazuri kwa kituo chetu,” alisema Dkt Mwakalago.

 Naye,Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kikuyu, Dkt  Azania Silliah alisema kuwa kata ya Kikuyu Kaskazini ina jumla ya wakazi 14,654 ambapo wanawake ni 9,250 na kati yao wajawazito ni  705.

“Kuanzia mwezi Julai mwaka jana (2023) mpaka kufikia  mwezi  Juni (2024), tumesajili na kuwapatia vyeti  watoto zaidi ya  642 sawa na asilimia 92%,” alieleza Dkt Silliah.

Mmoja wa wazazi waliopatiwa vyeti, Bi Halima Abdallah, mbali ya kuishukuru serikali kwa kazi nzuri inayofanya ikiwemo uboreshaji na ujenzi wa vituo vya afya, alisema uwepo wa huduma  hiyo inayotolewa  bure nchi nzima umekuwa mkombozi, kwani  kila mtoto anapata cheti cha kuzaliwa  mara baada ya  kuzaliwa  na hivyo  kuokoa gharama  ambazo zingezitumia kukipata kwenye ofisi za RITA.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Bw Frank Kanyusi alisema tangu zoezi hilo kusajili watoto wote chini ya miaka mitano watoto wengi wameweza kusajiliwa nchini nzima na mwamko umekuwa mkubwa.

“Naomba nikuhakikishie mheshimiwa Waziri kuwa RITA itahakikisha inamfikia kila mtoto anayepaswa kuandikishwa na kupata cheti cha kuzaliwa bure,” alisema Bw Kanyusi na kuishukuru serikali ya Awamu ya Sita chini Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na wadau wote wa maendeleo kwa kuunga mkono zoezi hilo

No comments:

Post a Comment

Pages