HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 02, 2024

CAMMAC yataka utekelezaji Mkataba wa Maputo


Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Faidha Selemani akizungumzia namna Jeshi la Polisi linavyopambana kuzuia ukatili ikiwemo kubakwa, ndoa za utotoni, kutoa mimba kinyume cha utarabu na zaidi kulinda raia na mali zao.

 
Na Irene Mark


MTANDAO wa Mashirika 13 yanayotekeleza Miradi ya  Afya ya Uzazi (CAMMAC) yameiomba Serikali kutekeleza vipengele muhimu ya Mkataba wa Maputo wa mwaka 2003 ili kuokoa waathirika wa ubakwaji na maharimu.

Wadau wa CAMMAC wamekutana jijini Dar es Salaam leo Julai 30,2024 kwenye kongamano la kujadili masuala ya haki za wanawake kwenye uzazi huku wakitaka Serikali kutekeleza maridhiano ya mkataba wa Maputo.

Akizungumza wakati wa kongamano hilo, Mkurugenzi wa Shirika la Uzazi na Malezi Bora (UMATI), Suzana Mkanzabi amesema umefika wakati sasa taifa litekeleze mkataba ule kwa vifungu vyote.

"...Mtu aliyebakwa na ndugu wa damu moja ikadhibitika na amepata ujauzo akaona si vema kuendelea kulea mimba hiyo aruhusiwe kisheria kuitoa kwa njia salama.

"Ukivaa viatu vya huyu muathirika utaona umuhimu wa jambo hili, vinginevyo harakati za utoaji mimba usio salama na vifo wakati wa kujifungua  hazitafanikiwa," amesema Mkanzabi.

Akizungumzia sheria za Tanzania, Wakili wa kujitegemea Baraka Thomas amesema hazilindi haki ya uzazi sababu mabinti na wanawake wanapoteza maisha kwa kutoa mimba isivyo salama kwa kuwa ni kosa kisheria.

"Suala la utoaji mimba linadhibitiwa kisheria... Kanuni ya Adhabu sura ya 16 inasema utoaji mimba bila sheria kufuatwa ni kosa la jinai, adhabu yake ni miaka 14 jela kwa mtu atakayemtoa mimba mwanamke au kama amejitoa mwenyewe pia atafungwa jela miaka saba," anasema Wakili Baraka.

Amesema sheria imepunguza miamya ya kutoa mimba isipokuwa kwa taarifa za daktari zinazoonesha kwamba mimba ile inahatarisha maisha ya mama.

Kwa majibu wa Wakili Baraka muathirika wa ubakwaji akiwemo aliyefanyiwa ukatili huo na ndugu wa damu moja akipata mimba anastahili kupata haki ya kuamua kuendelea nayo ama kuitoa.

Profesa Andrew Pembe wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na mtoa huduma za afya ya mama na mtoto amesema kesi nyingi za vifo vya uzazi historia yake wengi ni waliowahi kutoa mimba isivyo salama.

Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Faidha Selemani amesema Jeshi la Polisi linapambana kuzuia vitendo vya ukatili katika jamii kwa mujibu wa sheria ikiwemo kutoa mimba kiholela, ubakaji, ulawiti, mauaji na mengineyo.

"Tupo hapa leo kueleza nini jeshi tunafanya kwenye masuala ya mom ukatili hivyo tunaitaka jamii ishirikiane nasi kutokomeza matendo hayo," amesema ACP Faidha.

Hawa Mwaifunga Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Tabora amewataka CAMMAC, viongozi wa dini, Serikali na wataalam kuona nini cha kufanya kumsaidia mwananchi asiye na uwezo apate huduma ya kutoa mimba salama.

Mkataba wa Maputo unazungumzia haki ya afya ya mwanamke na uzazi ikiruhusu mwanamke kutoa mimba kwa njia salama ikiwa amebakwa na ndugu wa damu moja au mtu yeyote na ikathibitika mahakamani na kama hayupo tayari kuendelea kulea mimba hiyo.
 

No comments:

Post a Comment

Pages