Na Mwandishi wetu, Dodoma
SERIKALI itakazana kuona kwamba Tanzania inapotekeleza Mkakati wa Uchumi wa Kidijiti (2024-2034) vijana wengi waweze kuingia kwenye mifumo wa kidijitali ili wao wawe sehemu ya uchumi wa dunia wa kidijitali ambao unajengwa sasa.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk Moses Kusiluka, hapa wakati akifafanua kwa waandishi wa habari maazimio muhimu ya Mkutano wa 15 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) uliofianyika Ikulu Jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Mkutano umehimiza utekelezaji wa mkakati upewe kipaumbele.
“Serikali imejipanga, imekuja na mkakati wake kuhusu ujenzi mifumo ya kidijitali. Kwa hiyo tunaitia moyo sana sekta binafsi kuhakikisha wanatumia fursa hiyo; kuhakisha uchumi wetu unakuwa wa kidijitali na vijana wengi wanaingia kwenye mifumo kidijitali ili waweze kuwa sehemu ya uchumi wa kidijitali wa dunia,” alieleza Dr Kusiluka.
Kwa mujibu wa sensa ya 2022 Tanzania kuna idadi ya kuanzia miaka 15-24 jumla 11,848,365 sawa na asilimia 19.2 ya Watanzania wote; wanaume 5,657,379 na wanawake 6,190,986. Tanzania Bara vijana ni 11,463,718 ambao ni sawa na asilimia 19.2 ya wananchi wa Tanzania Bara. Tanzania Zanzibar vijana ni 384,647 sawa na asilimia 20.4 ya wananchi wa Tanzania Zanzibar.
Vijana 15-35 ni 21,312,411 sawa na asilimia 34.5 ya Watanzania wote. Bara vijana ni 20,612,566 sawa asilimia 34.4 ya wananchi wa Bara. Zanzibar ni 699,845 sawa na asilimia 37.0 ya wananchi wa Zanzibar.
Dk Kusiluka amesema kwamba kila mtu anaelewa kuwa dunia nzima inakwenda kwenye mabadiliko ya kidijitali. “Kwa hiyo sisi hatuwezi kubaki nyuma. Serikali imejipanga, imekuja na mkakati wake. Serikali itahusika na utekelezaji wake lakini sekta binafsi inapaswa kuangalia fursa katika hilo eneo kwa ajili ya kupanua chumi wetu,” alieleza kiongozi huyo.
Azimio lingine lilihusu kuandika Sera na Sheria ya Taifa ya Kuongeza ushiriki wa Wazawa katika Uchumi. Alieleza kwamba wafanyabiashara wanaona hawajashiriki sana katika miradi mikubwa ua kuna changamoto ya kushiriki. Mkutano ulibaini kuwa sababu kubwa ni kwamba sera na sheria bado havijakamilika. “Rais ameelekeza tukamilishe haraka sera ya hiyo ili kuwezesha wenyeji kushiriki vizuri katika uchumi, katika uwekezaji mkubwa, katika miradi mikubwa. Hilo tumejipanga kuhakikisha tunatekeleza ndani ya mwaka huu,” aliahidi.
Kuhusu kuimarisha mabaraza ya biashara ya TNBC ya wilaya na mikoa, Dk Kusiluka alisema mabaraza yataimarishwa ili iwe rahisi kuwakutanisha viongozi wa serikali na viongozi wa sekta binafsi ili watatue changamoto na kuweza kufungua fursa za uweekezaji na za biashara katika angazi za wilaya na mikoa kulingana na mazingira ya sehemu zao.
“Malalamiko yamekuwa ni kwamba kuna sheria ndogo ndogo zinazotungwa na halmashauri ambazo zingine zinakuwa kero; zinatofautiana kati ya sehemu na sehemu. Kwa hiyo ni muhimu mabaraza yajadili changamoto na utatuzi wake. Hata kama kuna za kuletwa juu, kama kuna haja kuletwa juu, ziletwe juu zikiwa zimechakatwa na viongozi wa serikali na wafanyabiashara ambao wanaonziishi,” alisisitiza.
Kuhusu azimio la kodi alisema Rais Samia tayari ameunda tume ya mabingwa ambao watatoa mapendekezo kwa serikali ili iyafanyie kazi.
Alieleza kuwa Rais Samia Suluhu Hasan alitoa tuzo kwa mikoa iliyofanya vizuri katika uendeshaji wa mabaraza, kuboresha mazingira ya biashara na ukusanyaji wa mapato ya serikali. Ameitaka mikoa mingine iige mifano ya mikoa iliyopata tuzo.
Katibu Mkuu Kiongozi,Balozi Dkt Moses Kusiluka akisitiza jambo kwa waandishi wa habari karibuni Jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment