HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 02, 2024

SIMBA, FISI WALA MIFUGO WADHIBITIWA

Mwandishi Wetu, Babati

WAFUGAJI wanaoishi ndani ya eneo la Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori ya Burunge (Burunge WMA) wilayani Babati, Mkoa Manyara na jirani na maeneo hayo, wamejengewa mazizi ya waya (Boma Hai) ili kuzuia wanyama wakali hasa Simba na Fisi kuvamia na kula  mifugo nyakati za usiku.

Mazizi hayo, yamejengwa na Taasisi ya Uhifadhi na Utalii ya Chem Chem, ambayo inafanya shughuli za uhifadhina na utalii katika eneo hilo, lilipo katikati ya hifadhi ya Taifa ya Tarangire na  Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara ikiwa ni sehemu ya mkakati wa taasisi hiyo, kupunguza migongano baina ya wanyamapori na mifugo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi mazizi hayo, Mkuu wa Wilaya ya Babati, mkoa wa Manyara, Lazaro Twange  amesema  mradi wa ujenzi mazizi hayo ni utekelezaji wa maagizo la serikali kupunguza migongano baina ya wanyamapori na binaadamu.

Twange ambaye aliwakilishwa katika uzinduzi wa mazizi hayo na Katibu Tawala wa Wilaya ya Babati, Khalfani Malipula amesema kazi nzuri ya uhifadhi imefanyika na sasa kuna changamoto ya wanyamapori kula mifugo jambo ambalo limeanza kupatiwa suluhu.

Amesema uzinduzi wa mazizi hayo, ambao umeambatana na maadhimisho ya siku ya Askari wa Hifadhi duniani (Rangers Day), unatarajiwa pia kuwaondolea wananchi adha ya kulala nje kulinda mifugo yao.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa zizi lake, John Bagary  mkazi wa kijiji cha Vilima Vitatu amesema, hadi juzi ng'ombe wake watano na mbuzi wanane walikuwa wameliwa na Simba.

"Nimekuwa nikilala nje kulinda zizi langu la ng'ombe na mara kwa mara Simba wamekuwa wakifika hapa usiku, lakini sasa nashukuru kujengewa zizi lenye uzio na taa za mwanga wa jua ili kuzuia Simba kuruka na kuingia ndani," amesema

Naye mkazi wa kijiji cha Ngoley, Peter Martin ameshukuru Chem Chem na Serikali kuwajengea mazizi hayo, kwani sasa watakuwa wanalala kwa amani.



Msimamizi wa Miradi ya Maendeleo ya Jamii ya Chem Chem, Napendaeli Wazoeli amesema Chem Chem kwa kushirikiana na askari wanyamapori, waliona katika maadhimisho ya siku ya askari wa wanyamapori duniani, kukabidhi mazizi hayo.

Amesema kila zizi limekuwa likigharimu zaidi ya sh milioni 2.6 na hadi jana mazizi 15 tayari yalikuwa yamejengwa na taasisi hiyo, ili kukabiliana na migongano baina ya wanyamapori na binadamu.

Katika maadhimisho hayo, Chem chem walitoa vifaa vya kufukuza wanyama katika makazi ya watu, ikiwepo baruti, vuvuzela, pilipili  na toshi maalum za kufukuza wanyamapori.

Akizungumza katika maadhimisho na uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori Burunge WMA, Erick Lilayoni amesema hifadhi hiyo, itaendelea kushirikiana na Chem Chem na wadau wengine ili kuhakikisha hifadhi inaendelea kuwa kivutio cha watalii.

Alisema wanaipongeza taasisi ya Chem Chem kwa msaada mkubwa ambao wamekuwa wakitoa katika jumuiya hiyo lakini pia kwa wananchi wanaishi ndani ya hifadhi hiyo.

"Leo tumeona askari wote wanaolinda hifadhi hii wamepewa medali na vifaa vya kufukuza wanyamapori , sisi tunaamini huu ni mwendelezo tu Chem Chem kusaidia uhifadhi katika eneo letu," amesema.



No comments:

Post a Comment

Pages