Afisa Usimamizi wa Fedha
kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha - Wizara ya Fedha, Bw.
Jackson Mushumba akitoa elimu ya Fedha kwa wanavikundi, wajasiriamali na
makundi maalum katika ukumbi wa Kilimanihewa mkoani Mtwara.
Baadhi ya wajasiriamali na
makundi maalum wa Kilimanihewa mkoani Mtwara wakipatiwa mafunzo ya
elimu ya fedha na Wizara ya Fedha wakishirikiana na Taasisi za Fedha
mkoani Mtwara.
Na Chedaiwe Msuya, WF, Mtwara
Wafanyabiashara wametakiwa kujenga tabia ya kuweka akiba katika biashara zao ili kuhakikisha wanakuwa na maendeleo endelevu.
Afisa
Sheria Mwandamizi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Ramadhani
Myonza, alitoa wito huo alipokuwa akitoa elimu ya utunzaji na matumizi
sahihi ya fedha katika ziara ya utoaji elimu ya fedha kwa umma wilayani
Masasi mkoani Mtwara.
Akitoa
elimu hiyo ya fedha, Bw. Myonza aliwasisitiza wafanyabiashara
kujiepusha na matumizi ya pesa zote wanazozipata na badala yake waweke
akiba ya sehemu ya mapato yao.
"Ndugu
wafanyabiashara, tujenge tabia ya kujiwekea akiba katika biashara au
katika mapato tunayopata katika utafutaji wetu." Alisema Bw. Myoka.
Alitoa
mfano wa mfanyabiashara anayepata shilingi laki moja, anashauriwa
kutumia shilingi elfu sitini na kuweka shilingi elfu arobaini kama akiba
kwani itamsaidia baadaye.
Aliwaasa
wafanyabiashara kuacha tabia ya kutumia pesa zote kwa kisingizio cha
kujipongeza, kwani kufanya hivyo kunawarudisha nyuma kimaendeleo.
Kaimu
Afisa Maendeleo ya Jamii, Bw. Ambros Ngwadakulima, eneo la Kilimanihewa
amewaeleza wananchi wa Mkoa wa Mtwara kutoa ushirikiano kwa wataalamu
na kuwaasa kujiunga katika vikundi vilivyokuwa rasmi, pia alisistiza
wale wote wanaotoa huduma za fedha kinyume na utaratibu wa kisheria
kuchukuliwa hatua.
Bi.
Maisha Raimondi, mfanyabiashara kutoka kijiji cha Makanga, alitoa
pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan, kwa kuwaruhusu wataalam kutoka Wizara ya Fedha kuzunguka
mikoani kutoa elimu ya utunzaji na matumizi sahihi ya pesa.
Alisema
kuwa elimu hiyo itawasaidia sana wafanyabiashara kuendesha biashara zao
kwa mafanikio na kuhakikisha kunakuwa na maendeleo endelevu.
Katibu
wa vikao, Bw. Ismail Rashidi, kutoka Kata ya Kilimanihewa, ameipongeza
Serikali kwa kutambua kuwa mkoa wa Mtwara kuwa miongoni mwa wanufaika wa
elimu hiyo.
Aliendelea
kusisitiza umuhimu wa wananchi wa Kilimanihewa kuacha tabia ya matumizi
mabaya ya fedha na kuwekeza katika taasisi zilizosajiliwa ili
kuhakikisha usalama wa fedha zao.
Afisa
Mkuu wa Bima kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Bi.
Gladness Lema, aliwahimiza wananchi kuwa na bima itakayoweza kuwasaidia
katika maafa mbalimbali yatakayojitokeza katika shughuli za kilimo na
kuweza kupata fidia kutokana na bima watakayoikata.
Wataalam
hao walisema kuwa Mtwara ni mkoa wa tisa tangu wameanza kutoa elimu
hiyo, wakitimiza maagizo ya Mhen. Rais kupitia Wizara ya Fedha kuzunguka
nchi nzima kutoa elimu ya fedha.
No comments:
Post a Comment