UKAME wa mabao unaomuandama straika wa kimataifa wa Zimbabwe, Prince Mpumelelo Dube, sio shida zao kabisaa mashabiki wa Yanga, wamemtia moyo kwa vitendo leo licha ya kutofunga bao katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar ya Manungu, Turiani, Morogoro.
Akicheza kama mshambuliaji kinara, kwa mara nyingine leo Dube ameshindwa kufumania nyavu, mbaya zaidi akipoteza nafasi kadhaa za wazi, lakini hilo halikuwatia unyonge mashabiki kwenye dimba la KMC Complex, jijini Dar es Salaam, ambao walimuita na kumchangia kiasi kikubwa cha pesa huku wakimtia moyo.
Wakicheza chini ya kocha mpya Pedro Goncalves, Mabingwa hao Watetezi wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, Yanga wameibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Wakata Miwa hao, shukrani kwa mabao ya mguu wa kushoto wa beki Mohammed Hussein 'Zimbwe Jr' na winga Celestine Ecua, waliofunga kwa mikwaju ya mbali nje ya boksi.
Kwa ushindi huo, Yanga ambao wamefuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, wamepanda hadi nafasi ya tatu ya msimamo wa Ligi Kuu wakifikisha pointi saba, moja nyuma ya Mbeya City na Mashujaa FC zinazoongoza zikiwa na pointi nane kila moja.
Kabla ya kuikandamiza Mtibwa Sugar leo, Yanga walishuka dimbani mara mbili kwenye mchakamchaka wa ligi hiyo inayojumuisha timu 16, ambako walianza kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Pamba Jiji, huku wakivuna sare tasa dhidi ya Mbeya City, kule Sokoine, jijini Mbeya.



No comments:
Post a Comment