HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 30, 2025

MCC RAJAB AIPONGEZA TUME HURU YA TAIFA YA UCHAGUZI

 Na Mbaruku Yusuph, Pangani


MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama (MCC), Rajabu Abdurhaman, ameipongeza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa kuweka utaratibu mzuri unaowawezesha Watanzania kupiga kura katika vituo mbalimbali nchini kwa amani na utulivu.
Rajabu alitoa pongezi hizo leo baada ya kushiriki zoezi la kupiga kura katika kituo cha Pangani Magharibi, Wilaya ya Pangani, ambapo aliungana na wananchi wengine kutimiza haki yao ya kikatiba ya kupiga kura.

Amesema kuwa ushiriki wa wananchi katika uchaguzi ni haki ya msingi ya kidemokrasia, hivyo ni muhimu kila mmoja kujitokeza ili kuwachagua viongozi wanaowataka kwa nafasi za Urais, Ubunge na Udiwani.

 “Nimejionea mwenyewe namna Tume ilivyojipanga kuhakikisha vituo vinafunguliwa mapema, na kwa kweli wameweka utaratibu mzuri unaorahisisha wapigakura kutekeleza wajibu wao bila usumbufu wowote,” alisema Rajabu.

Ameongeza kuwa hadi sasa hali katika vituo vya kupigia kura ni shwari, hakuna viashiria vya uvunjifu wa amani, na wananchi wanajitokeza kwa wingi kushiriki zoezi hilo muhimu kwa Taifa.

Rajabu amesema kwamba baada ya Pangani, anatarajia kutembelea maeneo mengine mkoani humo ili kufuatilia mwenendo wa uchaguzi na kubaini kama kuna changamoto zozote zilizojitokeza.

 “Kwa kweli niwapongeze sana Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC). Nimeuliza hapa na kuambiwa kuwa watu wanapiga kura kwa utaratibu mzuri. Hii ni hatua kubwa katika kuhakikisha kila Mtanzania anatimiza haki yake ya msingi bila vikwazo vyovyote,” aliongeza.

Aidha, Rajabu alikumbusha kuwa kabla ya uchaguzi, CCM ilifanya kampeni ya uhamasishaji katika mkoa mzima ili kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kushiriki uchaguzi kwa amani na utulivu.

Amewataka wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi kutokana na hali ya usalama na mshikamano uliopo, huku akisisitiza kuwa amani ni nguzo kuu ya maendeleo na msingi wa demokrasia yenye tija.

Kwa upande wake, Mwamtanga Kombora, mmoja wa wananchi wa Pangani, alisema kuwa vituo vya kupigia kura vilifunguliwa kwa wakati, na kwamba hakuna vurugu wala hali ya taharuki iliyoripotiwa.

 “Hali ya kiusalama imeimarishwa vizuri sana, hakuna fujo, na wananchi wanatekeleza haki zao za kikatiba kwa utulivu,” alisema Kombora.





No comments:

Post a Comment

Pages