Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuchukua hatua za haraka, shirikishi na zenye matokeo katika kukabiliana na changamoto za mazingira zinazoendelea kuikabili dunia.
Wito
huu umetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na
Watu wenye Ulemavu) Mhe. William Lukuvi katika hotuba aliyoitoa kwa niaba ya,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika
kikao cha ngazi ya juu cha Mkutano wa Saba wa Baraza la Mazingira la Umoja wa
Mataifa (UNEA-7), kinachoendelea jijini Nairobi, Kenya leo Desemba 11, 2025.
Katika hotiba hiyo, Mhe. Lukuvi alieleza kuwa
kaulimbiu ya mkutano huo inaakisi wazi changamoto kubwa za mazingira
zinazoukumba ulimwengu kwa sasa zikiwemo kupungua kwa bioanuwai, ongezeko la
uchafuzi wa mazingira, na shinikizo katika rasilimali asilia ni hali halisi
inayoathiri maisha ya mamilioni ya watu duniani.
“Dalili
za tahadhari ziko wazi kabisa. Hatuwezi tena kuziangalia kwa mbali. Tunahitaji
uongozi thabiti, unaotegemea ushahidi wa kisayansi na unaojengwa juu ya
mshikamano wa kimataifa,” alisema.
Akiainisha mwelekeo wa kimkakati wa Tanzania
katika mazingira, Mhe. Lukuvi alisema kuwa unaongozwa na Dira ya Taifa 2050,
Sera ya Taifa ya Mazingira, pamoja na Mikakati na Mipango mingine.
Aidha,
katika kufanikikisha mwelekeo huo, alibainisha kuwa Tanzania inaendelea
kuongeza matumizi ya nishati safi na salama, ikijumuisha nishati safi ya
kupikia, kuimarisha uhifadhi wa misitu, ardhi oevu na ukanda wa pwani; sanjari
na kuendeleza kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi.
Mhe. Lukuvi alisisitiza umuhimu wa ushirikiano
wa kimataifa katika kujenga uthabiti wa sekta ya mazingira, akisema kuwa hakuna
taifa linaloweza kujenga ustahimilivu peke yake bali unahitajika ushirikiano,
usawa katika upatikanaji wa teknolojia, pamoja na vyanzo vya fedha vya uhakika
na vinavyotabirika.
Halikadhalika,
alisema kwa nchi nyingi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania, changamoto za
mazingira mara nyingi huzidi uwezo wa kukabiliana nazo, hivyo, aliziomba nchi
washirika kutimiza ahadi zao katika kuzisaidia nchi hizo.
Pia, alisisitiza umuhimu wa kuwawezesha viongozi
wa sasa na wa vizazi vijavyo, hususan vijana, wanawake na wabunifu wa ndani
katika kusimamia hifadhi ya mazingira na kuhimiza mkutano huu uwe alama ya
mabadiliko, kuamua kuchukua hatua badala ya kusitasita, kuimarisha ushirikiano
badala ya mashindano na kuuendeleza uwajibikaji wa pamoja kuhusu maslahi
binafsi,
Mkutano
huo unaotarajiwa kuhitimishwa Desemba 12, 2025 unahudhuriwa pia na Naibu Waziri
Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Festo Dugange, Katibu
MkuunOfisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja na wataalamu mbalimbali
kutoka Ofisi hiyo.


No comments:
Post a Comment