HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

February 21, 2026

CRDB, HESLB na Baobab Link kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi wa kidijitali

BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu Tanzania imesema imeimarisha ushirikiano na sekta binafsi kwa lengo la kuongeza ushiriki wa vijana katika uchumi wa kidijitali na kuwajengea uwezo wa kujiajiri.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Upangaji Mikopo wa bodi hiyo, Dkt. Peter Mmari, amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya kuunganisha taasisi za umma na sekta binafsi ili kuongeza tija katika uwekezaji wa rasilimali watu.

“Muungano huu unalenga kuboresha huduma na kuongeza tija ya uwekezaji katika rasilimali watu,” amesema Dkt. Mmari.

Ameeleza kuwa tangu kuanzishwa kwa bodi hiyo mwaka 2004, zaidi ya Watanzania milioni 1.1 wamenufaika na mikopo yenye thamani ya takribani Sh trilioni 8.5, ikiwa ni sehemu ya uwekezaji mkubwa wa Serikali katika kujenga nguvu kazi yenye ujuzi na weledi.

Kwa mujibu wa Dkt. Mmari, maboresho ya mifumo ya kidijitali pamoja na usimamizi madhubuti yameongeza makusanyo ya marejesho hadi zaidi ya Sh. bilioni 220 kwa mwaka.

Katika kuimarisha zaidi ajenda ya uchumi wa kidijitali, bodi hiyo imeingia ubia na taasisi za Baobab Link na CRDB Foundation ili kuwawezesha wanafunzi kupata mafunzo ya ujuzi wa kidijitali, vitendea kazi pamoja na maarifa ya ujasiriamali.

Amesema ushirikiano huo utawawezesha wanafunzi kujiajiri wakiwa vyuoni na hata baada ya kuhitimu masomo yao, sambamba na kutumia kwa ufanisi mifumo ya mikopo inayotolewa na bodi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Foundation, Tullyesther Mwambapa, amesema taasisi hiyo itaendelea kutoa elimu ya fedha, ulezi na mafunzo ya usimamizi wa biashara ili kuhakikisha vijana wanatumia fursa hizo kuzalisha thamani na ajira.

Amesisitiza kuwa vijana ni nguvu kazi ya sasa na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali ni hatua muhimu ya kuharakisha ukuaji wa uchumi wa taifa.


 

No comments:

Post a Comment

Pages