BENKI ya CRDB imeingia makubaliano ya ushirikiano na CCBRT yenye lengo la kuimarisha ujumuishi wa kifedha na kuhakikisha huduma za benki zinawafikia watu wenye ulemavu na makundi mengine yenye mahitaji maalumu.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya CRDB, Dkt. Majid Nsekela, alisema hatua hiyo ni zaidi ya kusaini mkataba kwani inaonyesha dhamira ya benki hiyo katika kuhakikisha hakuna Mtanzania anayeachwa nyuma katika mfumo wa kifedha.
“Tunachofanya leo ni kuweka wazi msimamo wa CRDB kuhusu aina ya mchango tunaotaka kuutoa kwa jamii. Hii ndiyo inayotufanya kuwa tofauti, kwani tunaamini kuwa hakuna Mtanzania anayepaswa kuachwa nyuma katika huduma za kifedha,” alisema Dkt. Nsekela.
Alieleza kuwa mafanikio ya taasisi hayapimwi kwa kiwango cha faida pekee, bali pia kwa mchango wake katika maendeleo ya jamii. Kwa sababu hiyo, CRDB imeweka uwajibikaji wa biashara kuwa sehemu muhimu ya maamuzi yake ya kimkakati.
Dkt. Nsekela alisema ushirikiano huo unaendana na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), hususan SDG 1 ya kutokomeza umaskini, SDG 8 ya kukuza uchumi jumuishi na ajira, pamoja na SDG 10 ya kupunguza pengo la usawa.
Aidha, alisema benki hiyo imekuwa ikipokea ushauri kutoka kwa wateja wenye mahitaji maalumu ili kuboresha huduma zake na kwamba makubaliano hayo yatasaidia kutoa mafunzo, ushauri wa kitaalamu na tathmini ya mazingira ya kazi ili yawe rafiki kwa watu wenye ulemavu.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Dkt. Brenda Msangi, aliishukuru Benki ya CRDB kwa kuchukua hatua za makusudi katika kuwajumuisha watu wenye ulemavu kwenye huduma zake na katika maeneo ya ajira.
Alisema hatua hiyo inaonyesha dhamira ya kweli ya kujenga jamii jumuishi, huku akibainisha kuwa CCBRT imekuwa ikitekeleza programu mbalimbali za utetezi na ujumuishaji wa watu wenye ulemavu katika maendeleo.
“Tunaponena kuhusu kusimama na watu wenye ulemavu, tunamaanisha kutoa fursa sawa katika ajira, huduma na maendeleo. Ushirikiano huu na CRDB ni mfano mzuri wa namna sekta binafsi inaweza kushiriki katika kufanikisha azma hiyo,” alisema Msangi.
Kupitia ushirikiano huo, CCBRT itatoa msaada wa kitaalamu katika kufanya tathmini za ujumuishaji wa watu wenye ulemavu mahali pa kazi, kujenga uelewa kwa wafanyakazi, kutoa mafunzo kwa waajiri na kuboresha ufikikaji wa miundombinu katika maeneo ya kazi.
Makubaliano hayo yanatarajiwa kuongeza fursa za upatikanaji wa huduma za kifedha na ajira kwa watu wenye ulemavu, sambamba na kuimarisha usawa na maendeleo jumuishi nchini.




No comments:
Post a Comment