NA MWANDISHI WETU
BENKI ya CRDB kupitia CRDB Bank Foundation imetangaza maandalizi ya wiki ya kilele cha shughuli zake, huku matukio makubwa mawili yakitarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam, ikiwemo tamasha la iMbeju Sauti Moja na CRDB Bank International Marathon.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Mwambapa, amesema tamasha la iMbeju Sauti Moja Concert litafanyika Agosti 14, huku CRDB Bank International Marathon ikifanyika Agosti 16 katika Viwanja vya Posta.
Mwambapa amesema matukio hayo yanatarajiwa kuwa wikiendi ya burudani na michezo, huku washiriki wakipata fursa ya kujenga afya ya mwili na akili.
Amesema katika CRDB Bank International Marathon, benki hiyo imetenga jumla ya Sh milioni 120 kwa ajili ya zawadi mbalimbali, ikiwemo Sh milioni 12 kwa mshindi wa mbio za kilomita 42 kwa upande wa wanawake na wanaume.
“Kwa kiwango hicho cha fedha, hakuna mbio yoyote Tanzania ambayo imewahi kutenga Sh milioni 120 kwa ajili ya zawadi kama hizi,” amesema Mwambapa.
Kwa upande wake, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) imeungana na CRDB Bank katika mbio hizo za kimataifa, ikiwa na jukumu la kutoa burudani na vinywaji vya Castle Lite kwa washiriki na wageni.
Ushirikiano huo unalenga kuongeza hamasa na burudani katika moja ya matukio makubwa ya michezo yanayofanyika jijini Dar es Salaam.




No comments:
Post a Comment