NA MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM
CRDB Bank Foundation kwa kushirikiana na Kampuni ya Golden Star Consultants, imezindua ushirikiano kupitia Programu ya Imbeju unaolenga kuwawezesha vijana Watanzania kupata fursa za ajira, mafunzo na uzoefu wa kazi nje ya nchi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Biashara Changa wa CRDB Bank Foundation, Fadhili Bushagama, alisema ushirikiano huo unalenga kuwasaidia vijana wenye ndoto za kufanya kazi nje ya nchi lakini wanakabiliwa na changamoto za gharama za awali.
Alisema kupitia mpango huo, CRDB Bank Foundation itasaidia kugharamia baadhi ya mahitaji ya vijana wanaopata fursa hizo, ikiwemo tiketi za ndege, visa pamoja na malazi ya awali wanapowasili katika nchi wanazokwenda.
Kwa mujibu wa Bushagama, vijana hao watapata fursa katika maeneo mbalimbali ikiwemo kilimo na viwanda katika nchi za Ulaya, zikiwemo Denmark, Ujerumani na Uholanzi.
Alisema muda wa vijana kushiriki katika fursa hizo utatofautiana kuanzia miezi sita hadi miaka mitano, ambapo baada ya kurejea nchini wataweza kutumia ujuzi na uzoefu walioupata kuendeleza shughuli za kiuchumi, ikiwemo mashamba yaliyopo Morogoro.
“Lengo ni kuhakikisha vijana wanapata maarifa na uzoefu ambao watakaporejea nchini wataweza kuutumia kuendeleza shughuli zao, pamoja na kutoa ajira kwa vijana wengine,” alisema Bushagama.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Golden Star Consultants, Dk. Rehema Wandali, alisema kampuni hiyo imejikita katika kuwaunganisha vijana Watanzania na fursa za ajira, elimu na mafunzo ya vitendo nje ya mipaka ya Tanzania.
Alisema ushirikiano huo na CRDB Bank Foundation kupitia Programu ya Imbeju utasaidia vijana wengi kufikia fursa za kimataifa ambazo awali walishindwa kuzifikia kutokana na gharama za awali.
Dk. Wandali alisema mwaka 2026 kampuni hiyo inalenga kuwawezesha na kuwafikia vijana 1,500 kutoka mijini na vijijini kupitia fursa za ajira na mafunzo ya vitendo nchini Ujerumani, Canada, Sweden, Uholanzi na Denmark.
Aliongeza kuwa hadi sasa Golden Star Consultant imefanikiwa kuwaunganisha takribani vijana 500 na fursa katika sekta ya kilimo na mifugo.
“Wengi wamekuwa na vigezo na ndoto za kupata fursa hizi za kimataifa, lakini wamekuwa wakishindwa kutokana na gharama za awali kabla ya kusafiri. Ushirikiano huu utasaidia kuondoa changamoto hiyo,” alisema.
Alisema vijana watakaonufaika wataweza kupata maarifa, ujuzi, umahiri na uzoefu wa kimataifa pamoja na kujenga mitandao ya kitaalamu ambayo itawasaidia wanaporejea nchini kuchangia katika maendeleo yao binafsi, familia na taifa kwa ujumla.















No comments:
Post a Comment