NA MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM
SERIKALI imesema itachukua hatua za kisheria dhidi ya baadhi ya mawakala wa ajira nje ya nchi wanaowatoza vijana wa Kitanzania fedha nyingi kwa madai ya kuwawezesha kupata ajira na kusafiri kwenda kufanya kazi nje ya nchi.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Dkt. Evaline Munisi, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa huduma ya Ughaibuni Loan iliyoanzishwa na Benki ya CRDB kwa ajili ya kuwawezesha Watanzania wenye ajira zilizothibitishwa nje ya nchi, lakini wanaokosa fedha za kugharamia maandalizi ya safari.

Dkt. Munisi alisema huduma hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kupanua fursa za ajira, kuongeza kipato cha vijana na kuchochea mchango wa nguvu kazi ya Watanzania katika kukuza uchumi wa taifa.

Alisema Serikali haitavumilia vitendo vya utapeli vinavyofanywa na baadhi ya mawakala wa ajira, akieleza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kuwatoza vijana gharama zisizo halali.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa CRDB, Pendason Philemon, alisema benki hiyo imetenga zaidi ya Sh bilioni 250 kwa kipindi cha miaka mitano kwa ajili ya huduma hiyo.
Huduma hiyo inatajwa kuwa suluhisho kwa baadhi ya Watanzania wanaopata ajira zilizothibitishwa nje ya nchi lakini hushindwa kuondoka kutokana na kukosa fedha za maandalizi ya safari, ikiwemo gharama nyingine zinazohusiana na uhamaji wa kwenda kufanya kazi nje ya nchi.
Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Zuhura Yunuss, amewataka Watanzania kutumia fursa za ajira zinazopatikana katika soko la ajira la kimataifa.

Zuhura aliipongeza CRDB kwa kushirikiana na Serikali kutafuta suluhisho la changamoto za kifedha zinazowakabili Watanzania wanaopata ajira nje ya nchi.
“Leo hatuzungumzi mkopo pekee, bali tunazungumzia jambo pana zaidi linalogusa sera ya ajira, uwezeshaji wa vijana, ujuzi, uhamaji salama wa nguvu kazi, ujumuishaji wa kifedha na maendeleo ya taifa,” alisema.











No comments:
Post a Comment