NA EDITHA WILLIAM - KAGERA
Wafanyabiashara wapya mkoani Kagera wamepokea kwa matumaini mabadiliko yanayohusu msamaha wa kodi kwa kipindi cha miezi 12, wakisema hatua hiyo inaweza kuwa fursa muhimu ya kuimarisha biashara zao kabla ya kuanza kutimiza wajibu wa kulipa kodi.
BIASHARA wapya mkoani Kagera wamepokea kwa matumaini mabadiliko ya sheria za kodi yanayowapa msamaha wa kodi kwa kipindi cha miezi 12, wakisema hatua hiyo ni fursa muhimu ya kuwawezesha kuimarisha biashara zao kabla ya kuanza kutimiza wajibu wa kulipa kodi.
Kauli hiyo imetolewa wakati wa semina iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kagera kwa wafanyabiashara katika Ukumbi wa St. Teresa, Manispaa ya Bukoba, ikiwa na lengo la kutoa elimu kuhusu mabadiliko ya sheria za kodi yaliyomo katika Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Mfanyabiashara Jojina Jonathan Kagisa amesema msamaha huo wa miezi 12 ni fursa kwa wafanyabiashara wanaoanza biashara kupata muda wa kujipanga, kuimarisha shughuli zao na kujenga misingi imara ya biashara.
Amesema wafanyabiashara wanapaswa kutumia kipindi hicho kama muda wa maandalizi badala ya kukiona kama nafasi ya kukwepa wajibu wa kodi, ili baada ya kumalizika kwa miezi 12 wawe tayari kuanza kutimiza wajibu huo kwa ufanisi.
“Ni muhimu kutumia kipindi hiki kujenga uwezo wa biashara na kuweka mifumo mizuri, ili muda wa kulipa kodi unapofika mfanyabiashara awe tayari,” amesema Kagisa.
Kwa upande wake, mfanyabiashara Grace Pantaleo ameipongeza TRA kwa kuwakutanisha wafanyabiashara na kuwapatia elimu kuhusu mabadiliko ya sheria za kodi, akisema semina hiyo imewasaidia kufahamu fursa na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na mabadiliko hayo.
Grace amesisitiza umuhimu wa kuendelea kwa programu za elimu ya kodi ili wafanyabiashara wawe na uelewa wa kutosha kuhusu sheria na wasibaki nyuma katika utekelezaji wa wajibu wao.
Naye Meneja wa Chemba ya Taifa ya Biashara Mkoa wa Kagera, Rweyechungura Mali, ameipongeza TRA kwa kutoa elimu hiyo, akisema uelewa wa sheria za kodi ni muhimu katika kujenga mazingira mazuri ya biashara na kuwawezesha wafanyabiashara kutekeleza wajibu wao bila kuiona kodi kama kikwazo.
Mali ameitaka TRA kuchukua kwa uzito mapendekezo yatakayotolewa na wafanyabiashara na kuyafanyia kazi pale inapobidi, ili changamoto zitakazobainishwa ziweze kupata ufumbuzi.
Semina hiyo imekuwa pia jukwaa la mazungumzo kati ya TRA na wafanyabiashara, ambapo wadau wamepata fursa ya kuelewa mabadiliko ya sheria za kodi pamoja na kutoa maoni kuhusu namna bora ya kuboresha utekelezaji wake.
Wafanyabiashara wametoa wito elimu ya kodi iendelee kutolewa mara kwa mara badala ya kuishia kwenye semina moja, ili kila mfanyabiashara awe na uelewa wa haki, wajibu na fursa zinazotokana na sheria za kodi.



.jpeg)



No comments:
Post a Comment