KISARAWE, PWANI
KAIMU Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Nyahori Mahumbwe, ameishukuru Benki ya CRDB kwa kukabidhi meza na viti kwa ajili ya Shule ya Sekondari Muungano Boga, akisema msaada huo utasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Makabidhiano hayo yalifanyika mwishoni mwa wiki wilayani Kisarawe, Mkoa wa Pwani, ambapo Mahumbwe alisema hatua hiyo ni sehemu ya mchango wa CRDB katika kurudisha kwa jamii.

“Tunawashukuru sana Benki ya CRDB kwa moyo huu wa kujitolea kwenye jamii. ‘Giving back to society’ ni jambo jema sana mlilolifanya na ni sadaka pia,” alisema Kitare.
Alisema Halmashauri inaamini kuwa wanafunzi watakaotumia meza na viti hivyo watapata mazingira bora ya kujifunzia na kufanikiwa katika elimu yao, jambo ambalo pia litakuwa sehemu ya mafanikio ya wadau waliowezesha msaada huo.
Kitare pia alitoa wito kwa taasisi nyingine kushirikiana na Halmashauri ya Kisarawe katika kuboresha huduma za kijamii, hususan katika sekta za elimu na afya.
“Milango iko wazi, wahitaji wapo. Karibuni tushirikiane katika sekta mbalimbali za elimu na afya. Tukitekeleza haya tunamsaidia Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwahudumia Watanzania,” alisema.
Kwa upande wake Meneja Mahusiano Kanda ya Pwani, Idara ya Wateja wa Serikali Benki ya CRDB, Ian Kafuruki, alisema msaada huo ni sehemu ya jitihada za benki hiyo za kurejesha kwa jamii.
Alisema CRDB imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya kijamii katika manispaa na wilaya ambako benki hiyo inafanya biashara, huku sekta ya elimu ikiwa miongoni mwa maeneo yanayopewa kipaumbele.
“Benki ya CRDB imekuwa mdau mkubwa wa kuchochea maendeleo, hususan katika sekta ya elimu. Leo tupo hapa kutekeleza jitihada za Serikali za kuinua sekta ya elimu,” alisema Kafuruki.
Alisema meza na viti vilivyokabidhiwa vinatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo kwa wanafunzi na pia kuhamasisha wadau wengine kujitokeza na kuchangia katika kuboresha sekta ya elimu.
Kafuruki aliishukuru Halmashauri ya Kisarawe kwa ushirikiano wake na CRDB katika shughuli mbalimbali za kibiashara, akisema msaada huo ni sehemu ndogo ya kuonesha thamani ambayo benki hiyo inaipa jamii inayohudumia.
“Tunawashukuru sana Wilaya ya Kisarawe kwa fursa mbalimbali ambazo tumekuwa tukifanya nao biashara. Hii ni sehemu ndogo ya kurejesha na kuonesha jinsi gani tunawathamini na kutambua mchango wenu katika biashara,” alisema.






No comments:
Post a Comment