NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
BENKI ya CRDB na Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar zimesaini makubaliano ya ushirikiano yenye lengo la kusaidia taasisi za umma za kibiashara kuboresha uendeshaji, kupata mitaji na kutumia fursa mbalimbali za kifedha kwa ajili ya kuongeza tija.
Akizungumza katika hafla ya kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk. Abdulmajid Nsekela, alisema ushirikiano huo unalenga kuangalia namna ya kusaidia taasisi hizo, zikiwemo kampuni za Serikali Zanzibar, kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu usimamizi, fursa za uwekezaji na njia mbadala za kupata mitaji.
Alisema lengo la CRDB si kukopesha taasisi hizo pekee, bali kushirikiana nazo kubuni njia mbalimbali zitakazowezesha kuongeza tija katika uendeshaji wa shughuli zao na kupata mitaji kwa njia tofauti na mikopo.
“Ili tuweze kufanikiwa katika Dira ya 2050, sekta ya umma ni muhimu, hasa taasisi za kibiashara. Leo tumesema lengo letu si kukopesha, bali kushirikiana kubuni njia mbalimbali za kuleta tija katika uendeshaji wa shughuli zao na kuangalia namna wanavyoweza kupata mitaji tofauti na mkopo,” alisema Dk. Nsekela.
Alisema CRDB ina uzoefu katika kusaidia upatikanaji wa mitaji kupitia njia mbalimbali za kifedha, akitolea mfano Green Bond, Sukuk Bond na Samia Infrastructure Bond ambazo, kwa mujibu wake, zimefanikiwa kuvutia uwekezaji na kuelekeza fedha kwenye miradi maalumu.
Dk. Nsekela alisema ushirikiano huo pia unalenga kuleta mabadiliko chanya katika utendaji na usimamizi wa taasisi hizo ili kujifunza kutokana na mafanikio ya taasisi nyingine na kuongeza mchango wao katika uchumi.
“Tunataka kuangalia kwa nini wenzetu wamefanikiwa na sisi tusifanikiwe. Ninaamini kufanya haya kutakuwa sehemu ya mchango wa kutekeleza Dira ya 2050,” alisema.
Kwa upande wake, Msajili wa Hazina Zanzibar, Waheed Muhammad Ibrahim Sanya, aliishukuru CRDB kwa ushirikiano huo, akisema mchakato wa kufikia makubaliano hayo ulianza kipindi cha nyuma na sasa umefikia hatua ya kusainiwa.
Alisema Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar iko tayari kushirikiana na CRDB kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa, akibainisha kuwa makubaliano hayo yamepata baraka za Rais wa Zanzibar.
“Jambo hili tulikaa tukafikiria tulianze vipi. Ni mchakato ambao ulianza kipindi cha nyuma kidogo, na tunashukuru leo tumefikia kilele chake. Sisi kama ofisi tunashukuru na tupo tayari kufanya kazi na CRDB,” alisema Sanya.
Alisema atahakikisha timu iliyoundwa kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo inaendelea na kazi yake kwa ufanisi na kuja na maono pamoja na matokeo yanayotarajiwa.
Aidha, alisema mashirika ya umma yaliyopo Zanzibar yako tayari kushiriki katika utekelezaji wa ushirikiano huo kwa lengo la kuboresha utendaji na kuongeza tija.









No comments:
Post a Comment