Mbio zinazoenda kuongeza thamani ya Watu Wenye Uzito Mkubwa Michezoni
NA MWANDISHI WETU
UKIONDOA tambo za mashabiki wa Simba dhidi ya wale wa Yanga, hasa baada ya kuwachapa mabao 2-1 wikiendi iliyopita pale Uwanja wa Uhuru, gumzo la Jiji la Dar es Salaam kwa sasa ni uzinduzi na utambulisho wa Mbio za Heavy Weight Plus Size Maratho 2026.
Mbio hizo zitakazofanyika Desemba 27 mwaka huu jijini Dar es Salaam, zimezinduliwa Jumatatu ya Oktoba 12, likiwa ni tukio la kwanza, maalum na la aina yake nchini Tanzania na Afrika Mashariki na Kati, linaloenda kuongeza thamani ya Watu Wenye Uzito Mkubwa michezoni.
Waratibu wa mbio hizo zitakazofanyika chini ya kaulimbiu ya ‘Afya Yako ni Mtaji Wako, ni Kampuni ya Heavy Weight Sports Promotion chini ya Mkurugenzi Mtendaji wake, Tullo Chambo, ambao wanalitazama tukio hilo kama Jukwaa Huru Linaloenda Kuongeza Thamani ya Watu Wenye Uzito Mkubwa Michezoni.
MKURUGENZI MTENDAJI HEAVY WEIGHT AFUNGUKA
Linaitwa Jukwaa Huru kutokana na malengo waliyoweka waratibu hao ya kuzitumia mbio hizo kushirikisha hata watu wasio na uzito mkubwa, ili kurejesha ushirikiano baina ya makundi hayo katika jamii na kuvunja vitendo vya unyanyapaa dhidi ya watu wenye uzito mkubwa.
“Heavy Weight Plus Size Marathon ni mbio yenye utambulisho wa kipekee, iliyoanzishwa kwa sababu maalum ya kutoa fursa na mazingira rafiki kwa watu wenye uzito mkubwa, ambao mara nyingi hujisikia kutengwa, kubaguliwa na kutopewa nafasi ya kushiriki wa matukio ya kimichezo, hususani mbio.
“Kulingana na maono yaliyozaa Heavy Weight Plus Size Marathon, tunataka kulifanya tukio hili kuwa ni zaidi ya mbio, badala yake iwe harakati chanya na endelevu za kuhamasisha watu wenye uzito mkubwa kujikubali, kujiamini na kushiriki kikamilifu katika michezo, sambamba na kuunganisha jamii katika suala zima la mazoezi.
“Tukaona ipo haja ya kuyakutanisha makundi hayo yote, na kuyaweka pamoja na wadau wa michezo, wadau wa afya, familia, marafiki, watoto, taasisi, mashirika na jamii kwa ujumla, ambao wataenda kushindana katika mbio za Kilomita 15 (15KM Run), Kilomita 10 (10KM Run) na Kilomita 5 (5KM Run/Walk).
“Na katika kutekeleza malengo ya Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), ambalo linasisitiza kuwekeza kuanzia chini ili kuibua wanariadha wapya, tutakuwa pia na Mbio za Kilomita 2 na Nusu kwa Watoto (2.5KM Kids Run) na kategri ya mwisho ya mbio hizi itakuwa ni ya Fun Run Fitness Jog and Walk,” anafafanua Chambo.
SENSEI TAIFA LIWEWA: MICHEZO NI KWA WOTE
Heavy Weight Plus Size Marathon 2026 imezinduliwa na Mwakilishi wa West Coast Shotokan Karate Association Africa, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa West Coast Shotokan Karate Tanzania, Renshi Taifa Liwewa, huku akitoa wito wa watu kushiriki michezo bila kujali uzito au maumbile yao.
Alianza kwa kuwapongeza waratibu Heavy Weight Sports Promotion, kwa kuleta wazo hilo katika wakati muafaka Kabia, alioutaja kama uliogubikwa na magonjwa kibao nyemelezi yanayotokana na utamaduni hasi wa kutofanya mazoezi miongoni mwa watu wa uzito wote.
“Michezo na mazoezi ni kwa wote na kimsingi hayana mwisho katika maisha ya mwanadamu. Ukienda nchi za wenzetu, hsasa barani Asia, wazee miaka 90 wanakimbia asubuhi barabarani, wanafanya hivyo kujenga afya zao, ili kuiepusha miili yao na magonjwa kama mafua, kichwa, miguu kufa ganzi, nk.
“Magonjwa ambayo kama una uhakika wa mazoezi kila siku, ndio yatakujenga na kukuepusha nayo.
“Nimefurahi waratibu kuweka mbio za watoto, matukio mengi ya kimichezio tunawasahau hawa, tunapokwenda kutumia jukwaa hili kuwashirikisha watoto, tunaenda kujenga taifa imara na Madhubuti,” anasisitiza Liwewa.
Anaongeza kwa kuwashukuru pia waratibu kwa kuona umuhimu wa kujumuisha washiriki wasio na uzito mkubwa, kwa sababu wenye uzito mkubwa wakishindana wenyewe tu, watabweteka, akiamini kwamba wasio na uzito mkubwa watakuwa chachu ya wazito kushindana.
“Kupitia mbio hizi watu wajifunze kuamka mapema na kufanya mazoezi ya viungo. Wito wangu kwa wananchi wajisajili kwa wingi katika kategori mbalimbali.
Kipindi cha mbio hizi kitakuwa cha likizo, nitafurahi kuona wanafunzi na wanachuo wakijiandikisha kwa wingi,” anamaliza Liwewa.
KWANI WENYE UZITO MKUBWA WENYEWE WANASEMAJE?
Rais wa Big Mama Big Boss, ambaye pia ni Rais wa Vibonge Tanzania, Kippa Atugonza, ameipokea Heavy Weight Plus Size Marathon kwa furaha kubwa, akiamini kwamba jukwaa hilo linaenda kuvunja ngome za unyanyapaa miongoni mwa watu wenye uzito mkubwa katika ofisi na ajira.
“Big Mama Big Boss ni ‘movement’ inayowaunganisha Wamama Wanene ambao ndio Big Mama na Wababa Wanene ambao ndio Big Baba. Tulianzisha hii baada ya kugundua kuwa jamii inawanyanyapaa watu wenye uzito mkubwa kwenye usafiri wa umma na matukio mengine.
Kwa hiyo, Heavy Weight Plus Size Marathon tunaitazama kama inayokuja kuunga mkono harakati zetu za ukombozi wa watu wenye uzito mkubwa. Big Mama Big Boss tutashiriki kwa mapana, hili ni jukwaa letu na tutalitumia ipasavyo,” anasema Kippa Atugonza.
Msanii wa Bongo Movie, Lumole Matovolwa ‘Jobless wa Taifa’ maarufu pia kwa jina la Kobisi, ameshiriki uzinduzi huo na anadhani sasa ni wakati wa wao kuonesha kile wanachoweza kufanya bila kujali ukubwa wa miili yao na uzito wao mkubwa.
“Tunawashukuru waandaaji wa Heavy Weight Plus Size Marathon kwa kutuletea fursa hii muhimu ya sisi kushindana kwenye mbio, tumeshiriki sana marathon zisizo zetu, lakini wao wakaona ipo haja ya kutuletea mbio zetu na sisi. Hii sio ya kukosa.
“Nitashiriki kilomita 15 ya mbio hizi bila kukosa. Nimeshiriki Marathon mbalimbali nchini, zikiwemo za Dodoma Marathon, Msoga Marathon, Tulia Marathon na nyinginezo na nina medali ya mbio zote hizo. Tanzania mbio ziko nyingi, ila hizi sasa ndio zetu, hii ni ya kwetu,” anasema Kobisi.









No comments:
Post a Comment