Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Wateja 100 wa Benki ya CRDB wamejishindia Sh. 50,000 kila mmoja kupitia droo ya saba ya kampeni ya SimBanking Kimpango Wako, inayolenga kuongeza matumizi ya huduma za kibenki kwa njia ya simu za mkononi.
Aidha, wanafunzi watano wamejishindia simu janja (Smartphone), huku kundi jingine likihusisha wateja wanaotumia huduma za SimBanking kutoa fedha kupitia mawakala kwa miamala ya kuanzia Sh. 10,000.
Akizungumzia mwenendo wa kampeni hiyo, Meneja wa Huduma za Kibenki Kupitia Simu ya Mkononi wa CRDB, Amina Maona, amesema droo za kila wiki zitaendelea, ambapo washindi 50 wa kundi la miamala mingi, wanafunzi 10 na washindi 35 wa kundi la watumiaji wa mawakala watapata Sh. 20,000 kila mmoja.
Amesema kilele cha kampeni hiyo kinatarajiwa kuwa mwanzoni mwa Desemba mwaka huu, ambapo washindi watano watajishindia safari ya siku saba barani Ulaya.
Kwa mujibu wa Maona, CRDB itagharamia tiketi za ndege za kwenda na kurudi, malazi, chakula pamoja na bima ya safari, huku kila mshindi akipatiwa Sh. milioni moja kwa matumizi binafsi akiwa safarini.
CRDB imeendelea kuwahimiza wananchi kufungua akaunti na kutumia huduma za SimBanking kufanya miamala yao, huku wakipata fursa ya kushiriki katika kampeni hiyo na kujishindia zawadi mbalimbali.







No comments:
Post a Comment