NA MWANDISHI WETU
AFISA Michezo Manispaa ya Temeke, Mwajibu Chingwalu, amewataka nyota wanaounda timu ya Riadha ya Mkoa wa Dar es Salaam, inayoenda kushiriki Mashindano ya Wanawake ya Ladies First 2026, kujitoa kupambani ndoto na malengo yao, ikiwemo kuuheshimisha mkoa huo.
Michezo ya Ladies First 2026 inayotarajia kufanyika Novemba 27 na 28 - Kibaha mkoani Pwani, inaandaliwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), lengo likiwa ni kuwapa nafasi na kuhamasisha wanawake kushiriki riadha.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuiaga timu hiyo iliyoondoka jijini Dar es Salaam baada ya kuagwa, Chingwaru aliwataka wachezaji wakapambane, kuiwakilisha Dar, huku wakitambua kuwa juhudi zao michezoni ndio njia ya kuwapatia mafanikio katika nyanja hiyo.
“Mkifanya vizuri ‘Ladies First 2026, mnafungua fursa zingine zijazo baada ya mashindano haya. Mmetunzwa, mmefundishwa na mmetimiziwa mahitaji yenu, kapambanieni malengo yenu, ya kocha wenu na mkoa wetu kwa ujumla,” alisisitiza Chingwaru.
Afisa Michezo huyo aliwashukuru wadhamini wa timu hiyo Taasisi ya Alphonce Simbu Foundation na The Runners, kwa sapoti yao kubwa kufanikisha matunzo na mahitaji ya vijana wanne wanaounda timu ya mkoa wa Dar es Salaam inayoongozwa na Kocha Difna Chailla.
“Mliochaguliwa kuiwakilisha Dar mnapaswa kuithamini nafasi hii, mkoa una wakimbiaji wengi sana, kwahiyo msituangushe kwa kuwa mna dhamana ya kutuwakilisha.
“Vigezo vya uteuzi vilivyowapa nafasi hii, vinapaswa kupambaniwa na natamani mtakaporudi mje na medali ama vikombe hapa, nasi tujivunie uwakilishi wenu,” alisisitiza Chingwaru.
Awali akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Mkoa wa Dar es Salaam (DAA), Amani Ngoka, aliishukuru Serikali kwa kutoa baraka zake na kuiaga timu ya mkoa wake, akiamini thamani hiyo iliyooneshwa na Serikali italipwa kwa timu kuibuka na ushindi mshindanoni.
“Tunakushukuru Afisa Michezo kuja kuwaaga vijana wetu, tulikupa taarifa ya kushtukiza, lakini ukajitoa kuja kuwabariki vijana wetu. Timu hii itaondoka leo leo kuelekea kibaha, ikiwa na wachezaji wanne, kama taratibu inavyoagiza kila mkoa kutuma wachezaji wanne na kocha mmoja.
“DAA tunatamani kungekuwa na nafasi zaidi, kwani tuna nyota wenye umri huo wengi na bora, lakini kanuni zimetubana. Tuna Imani na wawakilishi wetu hawa, tunaamini tutatwaa vikombe vile vya ushindi wa nafasi tatu za juu kwenye kategori tofauti.
“Tunakuahidi timu ikirejea itakuja ofisini kwako kukabidhi vikombe na medali tutazotwaa katika Ladies First 2026,” alisema Ngokah uku akiwataka wachezaji kuhakikisha wanajituma mashindanoni na kuimarisha nidhamu na ari ya ushiriki.
Kwa upande wake, Kocha Mkuu, Difna Chailla aliishukuru DAA kwa kumuamini na kumpa timu hiyo na kwamba ingawa hawakuwa na matokeo mazuri katika Ladies First 2025, lakini tathmini za kina baada ya anguko lao mwaka jana na maandalizi bora, yanawapa uhakika wa ushindi mwaka huu.
“Mwaka jana DAA walinipa hii timu, hatukufanya vizuri. Tukakaa kufanya takafari na tathmini ya kipi kilitukwamisha, na ni matumaini yetu kwamba mwaka huu tutafanya vizuri kuliko ilivyokuwa 2025.
“Kama tulivyofanya katika Mashindani ya Riadha ya Taifa 2026, tukawa washindi wa pili kitaifa, basi matarajio ya kufanya vizuri zaidi huko Kibaha katika Ladies First yapo juu. Tunaamini tutakuwa na msahindano bora na tutarejea na ushindi,” alisema Difna.
Naye Nahodha timu hiyo, Shakira Karani, alisema yeye binafsi kama mkimbiaji wa mbio za mita 200, 400 na relay, amejiandaa vya kutosha kuweza kutwaa medali ya ushindi na kwamba ari iko juu miongoni nyota wenzake, ambao nao pia wana malengo chanya.
“Mimi kama mkimbiaji wa mita 200 na 400, nimejiandaa kufanya vizuri sana. Ninahidi ushindi, kinachonipa matumaini ni mafundisho ya kocha wetu, ambayo Tutayatumia vema kufanya vizuri zaidi katika mashindano haya kwa mwaka huu,” alisema Shakira kwa niaba ya wenzake
Afisa Habari wa DAA, Tullo Chambo, aliwataja nyota wanaoiwakilisha Dar es Salaam (na mbio zao kwenye mabano) kuwa ni pamoja nahodha Shakira (mita 400 na 800 na relay), Hellen Kagabo (mita 400, 800 na relay), Sharifa Mawazo (mita 100, 200 na relay) na Fauzia Ibrahim (mita 200, 400 na relay)
Chambo alisema DAA ina matumaini makubwa na wawakilishi hao na kwamba kama ambavyo mkoa wa Dar es Salaam ulivyovunja rekodi ya miaka 20 ya kuvurunda kwenye Mashindano ya Riadha Taifa na kushika nafasi ya pili, basi kuna kitu kikubwa kinaenda kufanywa katika Ladies First 2026.
“Mashindano ya Taifa 2026, tulivunja rekodi za usindikizaji kwa miaka 20, tukaibuka washindi wa pili kitaifa. Basi hiyo ni ishara kwamba tutatenda kufanya makubwa mwaka huu katika Ladaies First na kuzika jinamizi la kushika nafasi ya nane mwaka jana. Matarajio yetu mwaka huu ni kufanya vizuri zaidi,” alisema.





No comments:
Post a Comment