Leyla Mpinga, Dar es Salaam
Taasisi ya Waandishi wa habari za usaidizi wa jamii za pembezoni(MAIPAC) kwa kushirikiana na mtandao wa watetezi wa haki za Binaadamu(THRDC) amewataka wanahabari kuandika habari za Uchunguzi za Mazingira ili kusaidia jamii.
Wakifungua mafunzo ya siku mbili ya waandishi wa habari 35 wa mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani na Morogoro jijini Dar es Salaam, Mratibu wa kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo ole Ngurumwa na Mkurugenzi wa MAIPAC, Mussa Juma walitaka wanahabari nchini kubadilika na kuandika habari zenye matokeo chanya kuhusiana na mazingira.
Wakili Ole Ngurumwa alisema, kuna habari nyingi za uchunguzi zinapaswa kuandikwa lakini haziandikwi jambo ambalo linafanya wananchi wasiwe na taarifa sahihi za mazingira lakini pia kuleta uwajibikaji.
Ole Ngurumwa alisema, kwa sasa katika jiji la Dar es Salaam, kuna mkakati wa kuwaondoa wakazi wa Kata kadhaa wilaya ya Temeke ili kupisha maeneo ya kuhifadhi makontena ya mizigo kutoka bandarini, lakini hakuna habari za kina ambazo zimeandikwa ili jamii ifahamu mradi huo.
"Tuliambiwa Serikali ina mpango wa kufungua bandari za nchi kavu maeneo ya mkoa wa Pwani na kwingine ili kupunguza msongamano Dar es Salaam sasa kuna huu mpango mpya je tumefatilia kina nani wapo nyuma ya mradi huu"alisema.
Ole Ngurumwa alitaka wanahabari kwenda katika maeneo ya mradi huo, kupata maoni ya wananchi, viongozi wa serikali wa ngazi za chini, ili mradi huo usiwe na athari kwa jamii na mazingira kwa ujumla.
Wakili Ole Ngurumwa alisema tatizo la uchafu katika baadhi ya maeneo nchini na utupaji taka nguvu pembezoni mwa bahari bado lipo na wanahabari wanapaswa kuandika kwa kija ili kuokoa mazingira.
Kwa upande wake, Juma alisema mafunzo hayo ni mfululizo wa mafunzo kwa wanahabari nchi nzima, ambapo hadi sasa wanahabari 140 wamepatiwa mafunzo ya uandishi bora wa habari za mazingira lakini kujua sheria mbali mbali za mazingira.
Juma alisema, lengo la mafunzo hayo, ambayo yanadhaminiwa na Shirika la Umoja wa mataifa la UNESCO ni wanahabari kuandika vyema habari zente tija za mazingira ambazo zitarejesha uwajibikaji, utunzwaji wa mazingira na kufanyika maboresho ya sheria na Sera.
Alisema bado kuna migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji, migogoro ya wanyamapori na binadamu, ukataji mkubwa wa mikaa , kufyekwa misitu na uchafu wa mazingira lakini haziandikwi vya kutosha.
"Nyie ambao mmepata habari ya kuteuliwa katika mafunzo haya, kaandikeni habari za uchunguzi ili kuokoa jamii na dunia kwani hali sio nzuri na mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa na madhara makubwa"alisema
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya utetezi THRDC, Wakili, Paul Kisabo alianisha sheria zote za mazingira nchini ambazo wanahabari wanapaswa kuzifahamu na kuzitumia katika kuandika habari zao.
Wakili Kisabo alisema,kumekuwepo na changamoto za kuvunjwa sheria nyingi na hivyo kuchochea uharibifu wa mazingira lakini pia kuna udhaifu wa baadhi ya sheria na Sera hivyo, wanahabari wanapaswa kupaza sauti kudai sheria na sera bora za mazingira.
Akitoa mada katika mafunzo hayo, mwanaharakati wa mazingira, Deus Kibamba, aliwataka wanahabari kuandika habari za kina za uchunguzi, ikiwepo kufatilia ujenzi wa mahekalu pembezoni mwa bahari na uchafu uliopo katika maeneo hayo.
"Nendeni pembezoni mwa bahari ile sheria ya kuzuia ujenzi wa mita 60 karibu na bahari inatekelezwa na fatilieni kina nani wanamiliki hayo maeneo na je watanzania wa kipato cha chini wana nafasi gani ya kunufaika na fukwe za bahari"alisema.
MAIPAC na THRDC tayari wametoa mafunzo kwa waandishi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kati na tayari habari kadhaa za uchunguzi zimeanza kuripotiwa katika vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi.




No comments:
Post a Comment