HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 23, 2015

Watu sita washikiliwa kwa kukutwa na viungo vya Albino

Na Antony Sollo Shinyanga

JESHI la Polisi wilayani Kahama mkoani Shinyanga linawashikilia watu sita  kwa tuhuma za kukutwa na viungo vya Albino wakiwa katika harakati za kuviuza viungo hivyo.

Akizungumza Ofisini  kwake Mkuu wa kituo cha Polisi wilayani Kahama Leonard Nyandahu, alisema kuwa watu hao walikamatwa May 21 mwaka huu majira ya saa 7 mchana katika nyumba ya kulala wageni ya MAJI HOTEL, iliyopo katika maeneo ya Phantom kata ya Nyasubi wilayani Kahama. 

Nyandahu amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Bahati Kirungu(56) mwalimu wa shule ya msingi Katungulu kata ya Wendele, Wilayani Kahama ,Mhoja John(24) mkulima mkazi wa Isagehe Nzega,Biliya Busanda(39) mkulima mkazi wa Mogwa  Nzega.

Wengine ni Shija Makandi(60) mkulima mkazi wa Isagehe Nzega,Regina Kashinje(40) mkulima mkazi wa Isagehe Nzega,na Aboubakary Ally(25) ambaye ndiye aliyewahifadhi watu hao mkazi wa Isagehe Nzega.

Nyandahu amesema mnamo tarehe 19.5.2015 asubuhi mkuu wa upelelezi kituo cha Polisi Nzega alipata taarifa za mtu kuwa anauza viungo vya Albino na mtego wa kumkamata ulifanyika bila mafanikio badala yake akahamishia biashara hiyo wilayani Kahama.

Aidha Nyandahu amesema maafisa upelezi mkoa wa Tabora kwa kushirikiana na Afsa upelelezi kituo cha polisi Kahama walifuatilia nyendo za watu hao na ndipo mtego wa kuwakamata watu hao ulipowekwa na kuwanasa. 

Hata hivyo Jeshi la Polisi wilayani Kahama mkoani Shinyanga linaendelea kuwashikilia watu hao kwa mahojiano zaidi ikiwa ni pamoja na kuubaini mtandao huo ili waweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria

No comments:

Post a Comment

Pages