HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 14, 2017

Rais Magufuli ayatahadharisha magazeti kuhusu uchochezi Tanzania

Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli, ameyaonya magazeti mawili ambayo amesema yanaandika habari za uchochezi na kupotosha wananchi.
Amesema hatua ya magazeti hayo inahatarisha amani nchini humo.
Rais Magufuli ametoa onyo hilo wakati akikagua na kufungua kiwanda cha Jambo cha kuzalisha vinywaji baridi mkoani Shinyanga kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ikulu, kiongozi huyo amesema serikali haitayavumilia magazeti hayo mawili akisema yanaweza kuhatarisha amani ya nchi kama ilivyotokea katika nchini jirani ya Rwanda na kupelekea mauaji ya kimbari nchini humo.
''Serikali ya kutumbua majipu haiwezi kuacha kutumbua magazeti yanayofanya mambo ya uchochezi hatuwezi kuiacha Tanzania ikawa dampo la eneo la kuweka maneno ya uchochezi chini ya utawala wangu," alisema Dkt Magufuli.
"Hilo halitakuwepo kuna magazeti mawili tu kila ukisoma wao ni kuchochea tu ikizungumzwa habari hii wao wanageuza hii nasema na nataka wanisikie siku zao zimeshafika kama wanasikia wasikie wasiposikia wasisikie lakini magazeti mengine na vyombo vyote vingine vinatoa uchambuzi mzuri sana''.
Rais Magufuli amekuwa akikosolewa na baadhi ya wadau kwa tuhuma kwamba anakandamiza uhuru wa vyombo vya habari.
Baraza la Habari nchini Tanzania tayari limewasilisha kesi mahakamani kupinga Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari iliyopitishwa na bunge la nchi hiyo Novemba mwaka jana na siku chache baadaye ikatiwa saini na Rais Magufuli.
Mwishoni mwa mwaka jana, mwanzilishi wa mtandao wa Jamii Forums Maxence Melo alikamatwa na kushtakiwa kwa kukataa kufichua maelezo kuhusu watu wanaochangia kwenye mtandao huo.
Aliachiliwa huru baada ya kuzuiliwa kwa takriban wiki moja. BBC.

No comments:

Post a Comment

Pages