HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 21, 2019

Wakazi Kimaroroni wamlilia Waziri Lugola

Mzee Anthony Kalist Mbuya (69) na mwanaye Elvis Mbuya wakiwa wamelazwa katika hospital ya Kilema baada ya kuvamiwa na watu wanaodhaniwa  majambazi, Machi 18, Mwaka huu Kijiji Cha Kimaroroni Wilaya ya Moshi vijijini.

NA MWANDISHI WETU, MOSHI

WANAKIJIJI cha Kimaroroni Kata ya Kilema Wilaya ya  Moshi Vijijiji, mkoani Kilimanjaro wanamuomba Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, kuokoa maisha yao baada ya Jeshi la Polisi kushindwa kufanya hivyo hali iliyosababisha kukithiri kwa uhalifu na mauaji kijijini hapo.

Wakizungumza na Tanzania Daima kijijini hapo juzi, walisema licha ya juhudi binafsi za kujenga kituo cha polisi  wanaona hakiwasaidii kwa kuwa uhalifu haujapungua na askari polisi wawili waliopo kituoni hapo wanatuhumiwa kwa ulevi.

Kwa nyakati tofauti walisema askari polisi hao hawana silaha na kwamba hutoa taarifa za wasiri wao kwa wahalifu wakiwa kwenye vilabi vya pombe.

Kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini, walisema kati ya Januari mwaka huu na Machi 18 matukio matano ya wizi na raia kujeruhiwa kwa bunduki nabsilaha za jadi yamefanyika na taarifa kuripotiwa polisi bila watuhumiwa kukamatwa.

Walitaja baadhi ya matukio ya uhalifu waliyoyatolea taarifa na kupewa namba KIL/RB/253/2018 na KIL/RB/44/2019  na kwamba hawaoni hatua zinazochukuliwa na polisi.

''Matukio ni mengi na moja wapo ni la Machi 18 ambapo watu wanaodhaniwa majambazi walivamia nyumba ya Mbuya wakiwa na silaha mbalimbali, waliwajehi kwa kuwakata na mapanga maeneo tofauti ya mwili'' alisema mwanakijiji anayeishi jirani na Mbuya.

Alisema wanashindwa kuwataja wahalifu kwa madai polisi wanafichua siri huku pia wahalifu nao hujigamba kupata msaada wa kutolewa polisi kwani wanandugu ngazi za juu ikiwemo polisi na serikalini.

Kwa upande wao majeruhi wa tukio la ujambazi waliolazwa hospitali ya Kilema, Anthony Mbuya(69) na mwanaye Elvis Mbuya walisema walivamiwa saa 8 usiku na watu wenye silaha wakitaka fedha na walipokosa waliwajeruhi kwa mapanga.

''Ghafla nilisikia watu wapo ndani na waliingia na kukata umeme, baadaye walinikamata na kunishambulia kichwani na mikononi....sikujua nini kiliendelea maana nilipoteza fahamu'' alisema Mbuya. The fact

Naye  mwenyekiti wa kijiji hicho, Aloycia Lyaruu alithibitisha madai ya wananchi na kuongeza kuwa askari katika kituo hicho  hawana silaha na kushindwa kutoa msaada pale anapohitajika.

''Askari ukimgongea usiku kuhitaji msaada anachungulia kwanza dirishani na kama ni ujambazi anasema hana msaada wa haraka bali tuombe kituo cha polisi Himo....hata ingekua mimi nisingetoka'' alisema.

Mapema afisa mtendaji wa kijiji hicho,Eleuseri Asey, pamoja na kuthibitisha madai hayo alisema tayari wametoa taarifa mara kadhaa kuhusu matukio ya ujambazi na huduma hafifu ya polisi kituoni hapo.

''Wakati kituo cha polisi kinafungulia, mkuu wa jeshi la polisi nchini (IGP), Ernest Mangu aliahidi kituo kuwa na askari wasiopungua 16 lakini sasa hakuna jambo lililofanyika licha ya kukithiri kwa matukio ya ujambazi'' alisema.

Mkuu wa Wilaya hiyo na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Kippi Warioba aliahidi kufuatilia jambo hilo huku akisisiritiza kwamba hatua za makusudi za kuimarisha ulinzi kwenye Kijijini cha Kimaroroni zitachukuliwa.

Ofisa mwandamizi wa polisi ambaye siyo msemaji wa jeshi hilo, alithibitisha kuwapo kwa malalamiko kuhusu utendaji wa kituo cha polisi Kilema.

Alipotafutwa kwa njia ya simu yake ya kiganjani kwa ujumbe mfupi wa maandishi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah alisema wakazi wa mkoa huo wanajivunia hali ya Usalama iliyopo.

"Malalamiko yapi hayo na uhalifu uliokithili ni upi uliza mkazi wa kilimanjaro akueleze kama kweli kuna hali ya kukithili uhalifu moshi hatuwezi kupinga mtazamo wa mwananchi kudai uhalifu umekithili hasa kwa yule aliyetokewa tukio la uhalifu," alisema Kamanda Issah.

No comments:

Post a Comment

Pages