HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 08, 2013

LIONEL MESSI HANA MPINZANI TUZO YA BALLON D'Or


Lionel Messi akipunga mkono akiwa ameshikilia tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia. Kulia ni Rais wa Fifa Sepp Blatter

ZURICH, Uswisi

Messi, 25, alimbwaga mkali mwenzake klabuni Nou Camp Iniesta na hasimu wake na nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo katika kubeba tuzo hiyo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka ya Fifa

MSHAMBULIAJI Lionel Messi juzi usiku alivunja rekodi kwa kutwaa tuzo ya Ballon D’Or  kwa mara ya nne mfululizo – kisha akafungua mdomo kumwambia kiungo aliyemshinda Andres Iniesta: Nisingeweza kufanya vema kiasi hiki bila wewe.

Messi, 25, alimbwaga mkali mwenzake huyo klabuni Nou Camp Iniesta na hasimu wake na nyota wa Real Madrid Cristiano Ronaldo katika kubeba tuzo hiyo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka ya Fifa.

Na Messi nyota wa kimataifa wa Argentina, ambaye anakuwa mwanasoka wa kwanza kutwaa tuzo hiyo mara nne mfululizo duniani, alisisitiza kuwa ameyaweza yote katika msaada wa rafikiye huyo Iniesta.

“Ni jambo la kuvutia sana kupokea tena tuzo hii kwa mara ya nne mfululizo. Kila mmoja anastahili tuzo hii. Huwezi kuja hapa ukitambua na kufikiria kwamba ni wewe tu unayestahilio na kwamba unakuja kushinda.
 
“Ningependa kushirikisha furaha hii na nyota wengine wa FC Barcelona – hasa Andres Iniesta, ambaye yuko hapa na mimi.

“Najisikia fahari kubwa kufanya naye mazoezi kila siku. Mimi pia nawafikiria wachezaji wenzangu wa timu ya taifa ya Argentina.

“Shukrani za dhati kwa wote ambao walipiga kura kunichagua mimi kushinda tuzo hii, miongoni mwa manahodha, makocha wa klabu na makocha wa timu za mataifa mbalimbali.

“Shukrani zaidi ziifikie familia yangu, rafiki zangu na bila shaka kwa mke na mwanangu wa kiume, ambao kwao hiki kilichotokea kwangu leo ni kitu bora.”

Messi ameshinda tuzo hiyo katika mwaka aliofululiza kuvunja rekodi moja baada ya nyingine katika ulimwengu wa soka, akifunga jumla ya mabao 91 na kuivunja rekodi iliyodumu kwa miaka 40 ya Gerd Muller kufunga mabao 85 kwa kalenda ya mwaka.

Kocha wa timu ya taifa ya Hispania, Vicente Del Bosque alijishindia tuzo ya Kocha Bora wa Mwaka, akibebwa na ubingwa wa Mataifa Ulaya ‘Euro 2012’ katika fainali zilizopigwa nchini Poland na Ukraine mwaka jana.

Aidha, Abby Wambach, ambaye alifunga mabao matano katika mashindano ya Olimpiki jijini London, alitangazwa mshindi wa tuzo ya Ballon D’Or kwa wanawake, akifuata nyayo za Mmarekani mwenzake Mia Hamm aliyeshinda tuzo hiyo mwaka 2002.

No comments:

Post a Comment

Pages