NEW YORK, Marekani
“Ndiyo, msimu ujao
natarajia kurejea rasmi kuingoza klabu kama kocha. Sijui nitakuwa nafanya kazi
na timu gani, lakini natarajia kurejea rasmi kazini”
KOCHA wa zamani wa FC
Barcelona ya Hispania, Pep Guardiola amefungua milango kwa klabu za soka za
Ligi Kuu ya England kwa kudai kuwa: Natarajia kurejea rasmi katika soka msimu
ujao.
Na kauli hii ya kocha huyo
aneyesakwa zaidi duniani kwa sasa, imetajwa kama ashirio la wazi ya
kuzifungulia milango klabu za England zinazosaka saini yake za Chelsea,
Manchester City, Manchester United na Arsenal.
Guardiola, aliye mapumziko kwa
mwaka mmoja baada ya kukataa kurefusha mkataba wake Barcelona, alisema: “Ndiyo,
msimu ujao natarajia kurejea rasmi kuingoza klabu kama kocha. Sijui nitakuwa
nafanya kazi na timu gani, lakini natarajia kurejea rasmi kazini.”
Guardiola, ambaye anatarajia
kutimiza miaka 42 ya kuzaliwa kwake wiki ijayo, aliongeza: “Natarajia kurudi
kazini, kwa sababu mimi bado kijana. Niko vizuri sasa, naangalia mpira kama
shabiki na nafurahia kuona wachezaji mahiri.”
Inaeleweka kuwa kipaumbele cha
Guardiola kwa sasa anapofikiria marejeo yake katika soka ni kufanya kazi na
klabu za Ligi Kuu ya England.
Mmiliki wa klabu ya Chelsea,
bilionea Roman Abramovich hajaficha tama zake za kumpa mikoba Guardiola, huku
majaaliwa ya Mtaliano Roberto Mancini huko Etihad yaliko makazi ya Man City
yakiwa shakani.
Mkurugenzi mpya wa soka wa Man
City, Txiki Beguiristain, aliwahi kufanya kazi na Guardiola wakati akiwa
anainoa FC Barcelona.
Alex Ferguson hivi karibuni
alibainisha nia ya kubaki akiinoa Man United kwa miaka miwili ijayo – lakini
imeelezwa mapenzi na nia ya dhati ya kumuachia kiti hicho Guardiola, chagua
namba moja Old Trafford, inaweza kubadili mawazo ya Mskochi huyo.
Wakati huo huo, Arsenal inaweza
kuratibu jaribio la kufanya kazi na Guardiola kama mbadala wa Arsene Wenger,
iwapo ataamua kutimka klabuni hapo baada ya miaka 17.
Guardiola aliifundisha Barca
kwa mafanikio makubwa, akitwaa mataji 14 katika miaka minne ya uwapo wake Nou
Camp yaliko makazi ya vinara hao wa Lal Liga.
No comments:
Post a Comment