LUSAKA, Zambia
KOCHA wa mabingwa wa soka
barani Afrika, timu ya taifa ya Zambia ‘Chipolopolo,’ Herve Renard ametangaza
majina ya nyota 23 wa nchi hiyo watakaotetea ubingwa Mataifa Afrika nchini
Afrika Kusini waliotwaa Februari 2012, jijini Libreville, Gabon.
Renard amewaacha kikosini beki
mkongwe Chintu Kampamba, Salulani Phiri na Shadreck Malambo, katika orodha yake
aliyokabidhi kwa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) juzi Jumanne.
Saa chache kabla ya kutangaza
kikosi chake, Renard alimuita kikosini mlinda mlango Danny Munyau kujaza nafasi
ya Kalililo Kakonje, ambaye aliumia Jumapili kwenye mazoezi ya timu hiyo na
kuondoshwa.
Renard anaugulia vichapo vitatu
ilivyoambulia timu yake, katika mechi za majaribio dhidi ya timu za taifa za Tanzania,
Angola na Morocco, alizozitumia kupata wakali wa kikosi chake.
Keshokutwa Januari 12, Renard
mshindi wa tuzo ya Kocha Bora wa Mwaka barani Afrika, ataiongoza Chipolopolo
kucheza pambano la kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Norway, litakalopigwa
kwenye dimba la Levy Mwanawasa jijini Ndola.
Zambia itaanza harakati za
kuutetea ubingwa wao dhidi ya Ethiopia hapo Januari 21, kabla ya kuivaa Nigeria
Januari 25 na kumaliza mechi za makundi dhidi ya Burkina Faso hapo Januari 29
kwenye Uwanja wa Mbombela, mjini Nelspruit.
Kikosi cha Renard kinaundwa na
walinda mlango; Kennedy Mweene, Joshua Titima na Daniel Munyau, wakati mabeki
ni Stopilla Sunzu, Hichani Himonde, Francis Kasonde, Davies Nkausu, Joseph
Musonda na Emmanuel Mbola.
Viungo ni: Rainford Kalaba,
Nathan Sinkala, Mukuka Mulenga, Isaac Chansa, Chisamba Lungu, Felix Katongo,
Noah Chivuta na William, Njobvu, huku washambuliaji wakiwa ni Emmanuel Mayuka, Collins
Mbesuma, Jacob Mulenga, James Chamanga, Jonas Sakuwaha na nahodha Christopher
Katongo.
No comments:
Post a Comment