Na Bryceson Mathias
WATOTO ni taifa la kesho, ambalo likilelewa katika misingi na malezi bora kimaadili mema, lina nafasi kubwa ya kutoa viongozi waadilifu kama Rais, Mawaziri, Wabunge , Wakuu wa Mikoa, Wilaya na maneo mengine.
Pamoja na ukweli huo, Tanzania bado ina changamoto kubwa kwa watoto, hasa wanaoitwa wa mitaani ambao hawana makazi na wamekuwa wakirandaranda ovyo sehemu mbalimbali katika miji mikubwa kwa nia ya kutafuta namna ya kujikimu.
Kibaya zaidi, kama serikali hivi sasa haitakuwa makini na watendaji wake wanaohusika kushugulika na watoto hao wakabweteka, watoto wa mitaani nao wamenza kuzaa watoto wenzao wa mitaani, hivyo miji kuongeza watoto hao.
Katika miji mikubwa kama Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Mwanza, Mbeya na kwingineko, suala la watoto wa mitaani limekuwa la kudumu kwani kila kukicha watoto wanaongezeka katika mitaa hususani kando ya barabara kwa lengo la kuomba omba ili mradi mkono wao uende kinywani.
Kila kukicha watoto wa mitaani wanaongezeka, wanaweka kambi zao zisizo rasmi kwa nia ya kujihifadhi ili kuendelea na utafutaji wa riziki kinyume na taratibu na sheria zinazomsimamia mtoto kitaifa na kimataifa.
Katika siku za karibuni kumeibuka kina mama ambao ni wazazi ama walezi wa watoto hao, wakiwatuma watoto wao kwenda kusimama kando ya barabara kwa nia ya kuomba fedha ili kujikimu wao na familia.
Watoto hao wamekuwa wakiomba omba bila kujali athari mbalimbali, Kugongwa na Magari, Jua kali linalowachoma, Mvua inayowanyeshea, huku wazazi wao wakiwa wamekaa pembezoni mwa kuta au barabara ili kujikinga na jua au mvua jambo ambalo ni hatari zaidi katika ukuaji wa watoto hao.
kwao hii imekuwa kama ajira kwa watoto, ambao wanaanzia umri wa miaka mitatu, mpaka 15 ambapo walitakiwa wawe chini ya uangalizi wa walezi ama wazazi wao ili waweze kukua katika maadili mema na kusoma hatimae waje kulitumkia Taifa.
Jambo la kusikitisha, kutokana na udumavu huo wa kipato duni, watoto hao wamekuwa wkikumbana na kufanyiwa mambo mabaya ambayo mengine hata hayasemaki, licha ya ajira utotoni ambazo zimekuwa zikiwatharirisha huku watendaji wakikodorea macho bila huruma.
Si jambo la ajabu hususani kwa Jiji la Dar es Salaam na Miji mingine, kuona kila barabara utakayopita unakutana na watoto hao wakiwa wamejipanga wakinyoosha mikono na kukimbilia kwa kila gari linalosimama ili kujaribu bahati ya kupata riziki.
Mbaya zaidi utakuta kuna watoto wengine wanaelekea kwenye mapipa na mashimo ya Takataka wakiwa wamebebeshwa watoto wenzao mgongoni na kupanda nao katika vizingiti vya barabara kwa nia ya kuomba pasipo kujali hatari iliyopo ambapo wanaweza kuteleza pindi magari yanapokuwa yameruhusiwa kwenye taa au na askari wa Usalama barabarani.
Mimi najiuliza, hawa watu wa Ustawi wa Jamii wapo wapi? kama wapo wanfanya nini? Hii inaonesha Taifa na Kodi ya walalahoi inawalipa bila wao kupanga mbinu wala mikakati ya kuboresha ustawi wa Wizara yao inayohusika na mambo hayo, na maana nyingine Napata tabu na kichefuchefu cha uwepo wa mawaziri wizarani hapo, kwamba hawana ubunifu (creation) ya kumsaidia Rais na Taifa.
Pia nashindwa kuelewa kama mamlaka husika zinaliona na kulipa kipaumbele suala la watoto hao kwa kina, ambao katika hali ya kawaida walipaswa kuwa shuleni wakisoma ili kujenga maisha yao ya baadaye.
Sikatai, kuna watoto wengine wana wakati mgumu sana kutokana na wazazi wao kutengana ama kufiwa, hivyo kutokana na kukosa malezi na mahitaji muhimu, ambapo kwa shida wanazopata kwa walezi makatili, wanalazimika kujitafuria riziki zao kwa njia ya kuomba mitaani.
Ni wazi Wizara ya Wanawake Jinsia na Watoto, wakilichukulia suala hili kwa kina wanaweza kufanikiwa kuwakusanya watoto hao na kuwapatia msaada mbadala ili kuwawezesha kujenga maisha yao, kwani kwa muundo huu taifa linalojengwa hapo baadaye ni tegemezi na lisilo na maoteo.
Pia kuna kosa la Serikali kudhani kwamba mzigo huu ni wa taasisi za Dini na Taasisi zingine zikiwemo Asasi mbalimbali, japo ni kweli kwa upande mwingine lakini kunahitaji usimamizi na utalaam wa Watalaam wake ili kuzisaidia Taasisi hizi badala ya kuzitupia mzigo.
Nilipenda akina mama hao wanaowatuma watoto kuomba ni wazi kuwa wana chimbuko la walikotoka yaani sehemu maalumu, Serikali kupitia wizara na mamlaka husika wanapaswa kuingilia kati na kuwaondoa kwa nguvu ili kuokoa kizazi hicho kisipotee, kwani watoto hao wakiwa mitaani wanakumbana na changamoto ikiwamo kubakwa na mengineyo.
Serikali ni kama imewasahau watoto hao ambao hawajui hatari yoyote iliyopo mbele yao kutokana na kuwa na umri mdogo. Ni wazi watoto hao wakitafutiwa mahali pa kuishi na kupatiwa mahitaji muhimu hawatakuwa na sababu ya kuendelea kuomba.
Taifa hilo la kesho linapaswa kupatiwa elimu pamoja na mahitaji muhimu ili kujenga taifa imara na lenye misingi ya maadili yanayokubalika katika jamii. Kuishi kwa kuranda randa na kuomba mitaani hakuwezi kuzalisha taifa endelevu lenye nguvu na lenye mitazamo chanya ya kimaendeleo.
Si kweli kuwa suala la watoto mitaani Serikali imeshindwa kulitatua, zipo mbinu mbadala za kutumia ikiwamo kujenga kituo maalumu kwa ajili ya kukusanya watoto hao, ili kuwapatia mahitaji muhimu ikiwamo suala la elimu ili wasiweze kurudi mitaani.
Kama Serikali inaweza kutumia gharama kuwatawanya waandamanaji wanaodai haki, inaweza kuwahamisha watu kwenye makazi kwa kutumia vyombo na mitambo mikubwa yenye kuvunja na kuharibu nyumba za watu, inaweza kushindwa kudhibiti watoto wa mitaani na ombaomba wasiohitaji maji ya kuwasha, mabomu ya machozi na vurumai? Je tuseme hali hiyo pia inatokana na ukosefu wa utawala Bora?
Kwa mtazamo wangu naona kinachokosekana hapo ni kuwajibika kwa Mamlaka husika, ambazo bado zinauza sura nafasi zao za kazi. Kama Taifa linaweza kukimbiza mwenge nchi nzima na kuandaa sherehe za mamilioni ya fedha tutashindwa kuwaandalia mahali pazuri pa mafunzo kwa watoto hawa?
Fedha za Rushwa na Ufisadi katika chaguzi mbalimbali au fedha ambazo tumelipwa hivi karibuni toka nje Je, zisingeweza kuwajengeaa makazi watoto hawa na kuwafanya wawe na Babu yao wanayempenda kwa malezi wakiwa wanasoma?
Hii ni changamoto kwa wizara husika kufanya mikakati ya kutatua tatizo la ongezeko la watoto wa mitaani ambao kasi yao kila kukicha inaongezeka. Kwa Nia ya kuwaacha pasipo msaada wowote ili waendelee kuomba omba, kizazi kinachotengenezwa kitakuwa Ombaomba kutokana na kukosa mahitaji muhimu ikiwamo malezi na maadili mema.
No comments:
Post a Comment