HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 13, 2019

WAZIRI LUKUVI AFUNGUA MKUTANO WA MATUMIZI BORA YA RASILIMALI ARDHI NA UHIFADHI WA MANDHARI ZA AFRIKA, ARUSHA

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh. William Lukuvi (Mb) akifungua Mkutano wa Kimataifa kuhusu Matumizi Bora ya Rasilimali za Ardhi katika Mandhari ya Afrika (African Landscapes Dialogue) unaofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Arusha (AICC) jijini Arusha.
Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi Bw. Fidelis Mutakyamilwa akimkaribisha Waziri kwa ajili ya ufunguzi wa Mkutano huo.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) ambaye ndiye mwenyeji wa Mkutano huo Dkt. Stephen Nindi akitoa maelezo ya utangulizi kuhusu malengo na matarajio ya mkutano kabla ya kufuguliwa na Mh. Waziri
Mwakilishi wa Wizara ya Kilimo kutoka Serikali ya Uholanzi Bw. Hayo Haastra akitoa maelezo kwa washiriki namna Serikali ya Uholanzi inavyoshiriki kwenye mijadala ya matumzi ya ardhi katika mandhari mbalimbali za Afrika.
Mkurugenzi wa Eco Agriculture Sara Scherr, akitoa maelezo ya namna taasisi yake ilivyoshiriki katika maandalizi na kufanikisha kufanyika kwa Mkutano huo.
Mwakilishi kutoka Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) Boris Buechler akizungumza na washiriki kuhusu ushiriki wa Shirika hilo kwenye masuala mbalimbali ya matumizi ya rasilimali ardhi katika mandhari za Afrika
 Mwakilishi kutoka Senegal Chimmere Diaw wa African Model Forest Network akiwasilisha mada ya jinsi ya kusimamamia mandhari jumuishi ya matumizi ya ardhi
 Bwana John Recha kutoka programu ya mabadiliko ya Tabianchi akiwasilisha mada kuhusu upangaji matumizi ya ardhi katika mandhari mbalimbali kwa kuzingatia Sera na mabadiliko ya tabianchi
 Mkurugenzi wa Shirika la Solidaridad Afrika Mashariki na kati Rachel Wanyoike, akiendesha moja ya mijadala kuhusu matumizi ya ardhi katika mandhari mbalimbali za Afrika
 Washiriki wakifuatilia Mkutano
 Picha ya pamoja ya washiriki wa Mkutano wa Kimataifa kuhusu Matumizi Bora ya Rasilimali za Ardhi katika Mandhari ya Afrika (African Landscapes Dialogue. (Picha na Fredy Njeje).


Na Mwandishi Wetu 

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh. William Lukuvi, amefungua Mkutano wa Kimataifa kuhusu matumizi bora ya rasilimali ardhi kwenye Mandhari mbalimbali za Afrika wenye lengo la kujadili hali halisi na kubadilishana uzoefu katika upangaji, utekelezaji na usimamizi wa mipango ya matumizi ya ardhi katika Mandhari hizo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo Mh. Lukuvi amewapongeza Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kama muandaaji mwenyeji, Asasi zisizo za Kiserikali za Eco Agriculture Partners pamoja na wadau wengine wote waliofanikisha kufanyika kwa mkutano huo na Tanzania kuwa mwenyeji kwa mwaka huu.

Aidha, Mh. Lukuvi amewataka wadau hao kutoka ndani na nje ya nchi kushirikiana na kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa masuala mbalimbali ya kisekta yenye lengo la kuimarisha Mandhari Duniani hasa katika kipindi hiki ambacho mabadiliko ya tabia nchi yanazidi kushamiri na kuathiri uzalishaji na maisha ya binadamu katika maeneo mbalimbali Duniani.

Mkutano huo wa siku nne, unatarajiwa kujadili masuala ya uanzishwaji na utawala wa mandhari, utekelezaji na upangaji wa mandhari kwa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi, uimarishaji wa biashara, ajira na ujasiriamali katika uchumi wa kijani. Masuala mengine ambayo yanatarajiwa kujadiliwa ni pamoja na usimamizi wa wanyamapori na bionuai katika mandhari pamoja na udhamini kifedha, Uwekezaji, haki za miliki na matumizi ya ardhi katika mandhari. 

Inategemewa kuwa, kufanikiwa kwa utekelezaji wa masuala hayo yote katika nchi mbalimbali za Afrika na dunia kwa ujumla itakuwa ni chachu katika kuimarisha uchumi na kuleta maendeleo ya nchi na hatimaye kufanikiwa kwa malengo endelevu ya maendeleo (Sustainable Development Goals).

No comments:

Post a Comment

Pages